Mwanaharakati Stella Nyanzi afungwa miezi 18 kwa kumtusi rais Museveni

Mwanaharakati Stella Nyanzi afungwa miezi 18 kwa kumtusi rais Museveni

02 August 2019 Friday 16:50
Mwanaharakati Stella Nyanzi afungwa miezi 18 kwa kumtusi rais Museveni

Kampala, Uganda
MAHAKAMA nchini Uganda imemuhukumu  kifungo cha miezi 18 jela mwanaharakati msomi wa Uganda Dk Stella Nyanzi.

Hii leo Agosti 2, 2019 Nyanzi amepatikana na hatia ya unyanyasaji wa kimtandao pamoja na mawasiliano ya udhalilishaji dhidi ya rais Yoweri Museveni na familia yake.

Hata hivyo, Dk Nyanzi alikataa kumsikiliza hakimu akisoma hukumu dhidi yake na badala yake kufanya vurugu kwa kuvua nguo na kuonesha sehemu ya mwili wake.

Dk Nyanzi ambaye alikuwa ni mwalimu wa chuo kikuu cha Makerere nchini humo  na ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa rais Museveni , awali alishtakiwa kwa makosa mawili, unyanyasaji wa kimtandao pamoja na mawasiliano ya udhalilishaji rais Yoweri Museveni, na mkewe Janet Museveni pamoja na marehemu mama yake Museveni, Bi Esteri Kokundeka, kupitia ujumbe alioutuma kwenye Facebook.

Hata hivyo aliondolewa mashtaka juu ya mawasiliano ya udhalilishaji. Kesi yake iliendelea bila kuwepo mahakamani kwa mawakili wa Bi Nyanzi na hivyo kumuacha akijiwakilisha mwenyewe wakati wa hukumu dhidi yake.

"Ninaweza kujitolea kuukosa umama kwa chochote ninachotaka kukifanya . Nilizaliwa kwa ajli ya harakati hizi. Nitaongea kwa madikteta kwa kila lugha yoyote iwezekanayo," Dk Nyanzi alimwambia jaji anaesikiliza kesi yake, Gladys Kamashanyu.

Kulingana na sheria za Uganda, kosa la unyanyasaji wa kimtandao huadhibiwa kwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Nyanzi aliongeza angependa sana kupatikana na hatia ya makosa kwa sababu ni kweli alipanga kumtusi rais Museveni.

Nyanzi aliandika ujumbe wa matusi ya nguoni uliomuhusisha rais na marehemu mama yake , ambapo alisema kwamba rais Museveni alikufa wakati alipozaliwa.

Jaji aliuelezea ujumbe wa Facebook alioutuma, ambapo Bi Nyanzi alielezea mara kwa mara sehemu za siri za mama yake Museveni ,kuwa ulikuwa ni kinyume cha maadili, usio wa heshma na wa kuchukiza, mchafu na wenye matusi mabaya.

Nyanzi alikataa kuomba dhamana na yupo katika gereza kuu la Uganda la Luzira kwa miezi minane sasa.
Nchini Uganda, Bi Nyanzi amekua sura na sauti ya matumizi ya lugha chafu katika upinzani dhidi ya kile anachokiita serikali mbaya.

Haoni haya ya kuandika maneno ambayo wengi wanayaona kama ni ya aibu.

Awali alikamatwa na kuwekwa jela kutokana na ujumbe mwingine wa Facebook ambapo alimuelezea rais kama "makalio". Kesi juu ya mashtaka hayo bado inaendelea.
Nyanzi ni mtafiti wa masuala ya jamii na msomi na kabla ya kuanza kampeni yake ya matusi kupitia kwenye mitandao ya kijamii alikuwa ni mwalimu katika chuo kikuu cha umma nchini Uganda cha Makerere.

Mashtaka hayo chini ya sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta ni jaribio latika utekelezwaji wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni inayokosolewa.

Wengi miongoni mwa washukiwa wa unyanyasaji wa mtandaoni , wamekuwa hata hivyo wakishutumiwa kwa kumshambulia rais Museveni.

BBC

Updated: 02.08.2019 17:06
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.