Omar al Bashir asomewa mashtaka rasmi

Omar al Bashir asomewa mashtaka rasmi

17 June 2019 Monday 09:14
Omar al Bashir asomewa mashtaka rasmi

Khartoum, Sudan
ALIYEKUWA rais wa Sudan, Omar al-Bashir amesomewa mashtaka ya rushwa na ofisi ya mwendesha mashtaka wa nchi hiyo.

Inakuwa ni mara ya kwanza kwa Bashir kuonekana hadharani tangu kuondolewa kwake madarakani mwezi Aprili, 2019. 

Akiwa amezungukwa na askari wa usalama, akitoka gerezani kiongozi huyo wa zamani  (75) alikua amevaa vazi lake jeupe na kilemba.

Alipinduliwa madarakani baada ya miezi kadhaa ya maandamano nchini humo.

Waendesha mashtaka wanasema kuwa maburungutu ya fedha za kigeni yalikutwa kwenye magunia nyumbani mwake baada ya kuondolewa madarakani alikohudumu kwa takribani miaka 30.

Bashir alionekana akishuka kwenye gari kuingia kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka, akitabasamu na kuzungumza na walinzi, lakini baadae alirejea akiwa na uso usio na furaha, Shirika la Reuters limeeleza.

Pia Bashir anatakiwa na mahakama ya kimataifa, ICC, akishutumiwa kuongoza vitendo vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu katika eneo la Darfur, shutuma ambazo amezikana.

Wakati huohuo, Mohamed Hamdan ''Hemeti'' Dagolo,ambaye ni makamu wa rais wa jeshi la junta ameahidi kuwafikisha mbele ya sheria watu waliofanya ghasia za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa wanaharakati wa upinzani, zaidi ya watu 100 waliuawa  Juni 3, vikosi vya Sudan vilimaliza maandamano baada ya waandamanaji kupiga kambi makao makuu jeshi wakidai utawala wa kiraia.

Mamlaka ya jeshi la Sudan, limekuwa likikosolewa na mataifa duniani kuhusu namna walivyokabiliana na waandamanaji.

Sudan imeondolewa uanachama wa Umoja wa Afrika.

Siku ya Ijumaa baada ya kutembelea Khartoum,mjumbe wa Marekani barani Afrika, Tibor Nagy ametaka kufanyike uchunguzi kuhusu mauaji yaliyotekelezwa.

Mazungumzo kati ya waandamanaji na Baraza la kijeshi yalivunjika baada ya ghasia kutokea.

Updated: 17.06.2019 09:47
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.