Wapinzani waandamwa Burundi

Wapinzani waandamwa Burundi

14 June 2019 Friday 12:12
Wapinzani waandamwa Burundi

Bujumbura, Burundi
SHIRIKA la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake kuwa maafisa wa serikali ya Burundi na vijana wa Imbonerakure wanahusika na kuwapiga,kuwakamata kiholela, kupotea na kuuwawa wapinzani.

 Kampeni ya kuwaandama watu wanaotuhumiwa kukipinga chama tawala imekuwa ikiendelea tangu kura ya maoni ya katiba ilipoitishwa Mei 2018. 

Hata hivyo kampeni hiyo inaonyesha kuzidi makali tangu chama kipya cha upinzani kiliposajiliwa mwezi wa Februari 2019.

Wanachama wa Imbonerakure, jumuiya ya vijana wanaoshirikiana na chama tawala cha CNDD-FDD na wakuu wa serikali za mikoa wanaendelea kuwashinikiza raia na hasa wa mashambani wajiunge na chama tawala mnamo wakati huu ambapo Burundi inajiandaa kwa uchaguzi wa rais mwaka 2020. 

 Shirika la Human Rights Watch linasema katika ripoti yake vijana wa Imbonerakure na viongozi wa serikali za mikoa wanawaandama wanachama wa chama kipya cha "Baraza la taifa kwa ajili ya Uhuru-CNL katika mikoa isiyopungua minane kati ya 18 bila ya kuhofia adhabu yoyote.

Lewis Mudge, mkurugenzi wa Human Rights Watch kwa eneo la Afrika Kati anasema matumizi ya nguvu yanayozidi kukithiri yamesababishwa na hali ya watu kutojali sheria ikiyoko nchini Burundi.
Amevitaja visa vilivyoripotiwa kuwa ni sehemu ndogo tuu ya visa vinavyotokea na ambavyo haviripotiwi kutokana na kutokuwepo vyombo huru vya habari na mashirika ya kijamii.

Kati ya mwezi wa Februari hadi Mei, 2019 shirika la Human Rights Watch limefanya mahojiano 33 kwa njia ya simu pamoja na wahanga, familia zao na mashahidi wa visa vilivyotokea katika mikoa ya Babanza, Cibitoke, Gitega, Karusi, Kirundo, Muramvya, Muyinga, Ngozi na Rumonge pamoja pia na katika mji mkuu Bujumbura. 

Zaidi ya hayo wachunguzi wa shirika hilo linalopigania haki za binaadam wamewahoji watu 30 walioipa kisogo Burundi baada ya kura ya maoni ya Mei mwaka jana.

Visa visivyopungua vitatu vya mauwaji, vinne vya watu wasiojulikana waliko na 24 vya watu waliokamatwa kiholela vimeorodheshwa na Human Rights Watch katika mikoa hiyo minane ya Burundi tangu Januari mwaka huu. 

Zaidi ya hayo kuna kadhia za mauwaji ya watu 3 na mmoja ambaye hajulikani aliko zilizoripotiwa na shirika hilo la haki za binaadam baada ya Mei 2018 nchini Burundi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kesho kuzungumzia hali inayozidi kua mbaya nchini Burundi.

DW

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.