Bunge laridhia mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki

Bunge laridhia mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki

11 September 2019 Wednesday 15:14
Bunge laridhia  mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki

Na mwandishi wetu, Dodoma

SERIKALI imesema inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 33 ya wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini, wameathiriwa na Zebaki kwa kupata magonjwa yakiwemo yale ya mifumo ya neva za fahamu, uzazi, upumuaji, figo, moyo, na udhaifu wa mwili.

Akiwasilisha azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) George Simbachawene amesema, baadhi ya athari kwa mazingira zilizobainika kutokana na matumizi ya zebaki ni pamoja na kudhoofika kwa ukuaji wa viumbe hai wanaoishi ndani ya maji; uchafuzi wa mfumo mfuatano wa mazao ya chakula, mifugo na samaki; na uchafuzi wa vyanzo vya maji, hewa na udongo.

“Lengo kuu la Mkataba huu ni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya Zebaki katika hatua za uzalishaji, matumizi na utupaji wake,” alisisitiza Simbachawene.

Simbachawene ameainisha sheria ambazo zinatoa mwongozo wa jumla kuhusu usimamizi wa Zebaki ikiwa ni pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004); Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani (2003); Sheria ya Madini (2010); Sheria ya Afya ya Jamii (2009); Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (2003); na Sheria ya Chakula na Dawa (2003) na kusisitiza kuwa zitaandaliwa kanuni za Usimamizi wa Zebaki chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004) ili kuwezesha utekelezaji wa Mkataba huu.

Tafiti zinaonyesha kuwa zebaki hudumu katika mazingira kwa muda mrefu (miaka 2 hadi 20) na husafiri masafa marefu kwa njia ya hewa, maji (mito, maziwa na bahari) na udongo umbali hadi kilomita 1,000 kutoka kwenye chanzo; na kuathiri afya ya binadamu, viumbe wengine na mazingira. Athari hizi zinajitokeza zaidi katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea kutokana na nchi hizo kupunguza matumizi ya Zebaki.

Awali akiwasilisha hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Suleiman Ahmed Sadiq amesema Kamati inaona umuhimu wa nchi kuridhia Mkataba huu kwa lengo la kushirikiana na nchi nyingine kutafuta suluhisho la zebaki bila kuathiri shughuli za wachimbaji wadogo.

“Ushauri wa Kamati ni kuwa Serikali ijitahidi kuhakikisha inapatikana teknolojia rahisi na rafiki kwa wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu” alisisitiza Sadiq.

Zebaki ni miongoni mwa kemikali zinazohatarisha zaidi afya ya jamii duniani kutokana na kudumu katika mazingira kwa muda mrefu, kusafiri masafa marefu kwa njia ya hewa, maji (mito, maziwa na bahari) na udongo na hivyo kuathiri afya ya binadamu na mazingira.

Jumla ya nchi 113 zimeridhia Mkataba huu ambao ulianza kutekelezwa rasmi Agosti 16, 2017 mara baada ya Nchi 50 kuridhia kama inavyotakiwa na Ibara ya 30 ya Mkataba wa Minamata.

PICHANI: Wachimbaji wadogo wa dhahabu wakichejua dhahabu kwa kutumia zebaki hali ambayo si tu inahatarisha afya zao bali pia mazingira.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.