Waziri ashtukia matumizi milioni 60 aagiza uchunguzi ufanyike

Waziri ashtukia matumizi milioni 60 aagiza uchunguzi ufanyike

12 July 2019 Friday 15:29
Waziri ashtukia matumizi milioni 60 aagiza uchunguzi ufanyike

Na mwandishi wetu, Morogoro

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ameagiza uchunguzi ufanyike wa matumizi ya milioni 60 zilizotumika kununulia dawa ya mchwa  katika jengo la Hospital ya Wilaya ya Morogoro linaloendelea kujengwa katika eneo la Mvuha.

Pia amesema kwa kipindi kirefu halmashauri ya Morogoro imekuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo hali hiyo inaonyesha dhahiri kuwa kuna changamoto ya kiungozi. 

Jafo alihoji matumizi hayo baada ya kutoonekana kwa kipengele hicho kwenye taarifa ya matumizi za fedha za ujenzi wa hospital hiyo pamoja na gharama kubwa iliyotumika kununulia dawa hizo. 

Akiwa katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa hospital za Wilaya ya Morogoro  Jafo alipokea taarifa ya ujenzi yenye mchanganuo wa matumizi ya fedha zaidi ya Bilioni moja ilihali kipengele cha ununuzi wa dawa hizo za mchwa uliotumia zaidi ya milioni 60 kutoonekana kwenye matumizi yaliyowasilishwa. 

Jafo alihoji endapo dawa ya kudhibiti mchwa iliwekwa kwenye majengo hayo na kujibiwa kuwa ndio na kazi hiyo ilifanyika kwa gharama ya  milioni 60 ndipo alipouliza kwanini matumizi ya fedha hizo hayajawekwa kwenye taarifa. 

“Bei ya ununuzi wa dawa hiyo si halisi na sijui kama mlijaribu kujilinganisha na wenzenu wa halmashauri nyingine ili mfahamu kuwa walitumia kiasi gani kwenye ununuzi wa dawa kama hiyo ni kiasi gani au ninyi mmenunua dawa ya aina gani ambayo imegharimu kiasi hiki kikubwa cha Fedha” Alihoji Jafo. 

Jafo aliongeza  "Kama mlinunua dawa hiyo kwanini matumizi ya fedha hizo hayaonekani kwenye taarifa yenu, napata mashaka na matumizi ya fedha hizo hapa ni lazima ije timu maalumu kwa ajili ya kuchunguza matumizi mabaya ya fedha za Mradi wa Ujenzi wa Hospitali hii''. 

Wakati huo huo Jafo alisema kuwa kwa kipindi kirefu halmashauri ya Morogoro imekuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo hali hiyo inaonyesha dhahiri kuwa kuna changamoto ya kiungozi. 

“Hapa kuna tatizo kubwa na lazima tulipatie ufumbuzi haiwezekani nyie mara mnashindwa kutekeleza miradi kwa wakati kuanzia ujenzi wa Jengo la Halmashauri shilingi milioni 500 hazijulikani zilipo na mpaka leo Jengo halijajengwa sasa mnataka tena tabia hiyo muilete kwenye mradi wa Hospital safari hii mtamaliza ujenzi huu haijalishi fedha mnazo au mmezitumia ni lazima mkamilishe ujenzi. 

"Mpaka sasa mmekwishatumia  bilioni moja  kujenga majengo haya ambayo hayaridhishi na hamjafikia hata kwenye hatua ya kupaua huku mnaniambia mmebakiwa na milioni 400 sitaki kusikia sababu yeyote ninachotaka ni kuona ifikapo Julai 30 Hospital hii imekamilika” alisema Jafo. 

Akitolea ufafanuzi changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa hospital ya Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama imekuwa ikishauri kila wakati namna bora na ya haraka ya kukamilisha mradi huo lakini kumekua na muitikio mdogo wa wataalamu wa Halmashauri katika kutekeleza yale yanayoshauriwa na Kamati hiyo. 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Masoud Rioba alifafanua manunuzi ya dawa za kuua mchwa kuwa yalijumuishwa kwenye taarifa ya mradi katika kipengele cha vifaa vya ujenzi na sio kwenye kipengele kinachojitegemea ndio maana sio rahisi kuiona kwa uharaka. 

“Manunuzi ya dawa yamejumuishwa kwenye vifaa vya ujenzi haionekani kwa haraka kwa sababu hatukuiweka peke yake na gharama yake ni shilinngi milioni 60 hii ni baada ya kununua lita 1500 ambazo ndizo zilizokuwa zinahitajika na kila lita moja ilikua na gharama ya zaidi ya shilingi elfu 55 hivyo kuleta gharama ya zaidi ya shilingi milioni sitini,” alisema Rioba. 

Akifafanua kuhusu fedha zilizobakia kama zinaweza kukamilisha ujenzi wa Hospital hiyo amesema mpaka sasa vifaa vingi vimekwishanunuliwa hivyo fedha hiyo iliyobakia itaweza kufanya kazi za ukamilishaji wa majengo hayo na amemuhakikishia Mhe. Waziri wa Nchi kuwa kazi hiyo itakamilika kwa fedha zilizobakia. 

Wakatihuo huo mmoja wa mafundi wanaotumika katika kazi za ujenzi wa hospital hiyo amelalamika kukosekana kwa vifaa vya ujenzi kwa muda mrefu katika Hospitali hiyo huku malipo ya mafundi hao yakisuasua kitu kilichoplekea kuwakatisha tamaa na morali wa kuendelea kufanya kazi hiyo. 

PICHANI JUU; Kutoka Kushoto ni Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Kebwe Steven Kebwe, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo na Mkurugenzi wa Morogoro, Masoud Rioba wakifuatilia taarifa ya matumizi ya fedha za ujenzi wa hospital ya Morogoro wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo. 

PICHA CHINI; Muonekano wa moja ya majengo ya Hospital ya Wilaya ya Morogoro 

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.