banner68

Hadithi za kutisha za ubakaji, kukata shingo Sudan Kusini

Hadithi za kutisha za ubakaji, kukata shingo Sudan Kusini

11 July 2018 Wednesday 09:39
Hadithi za kutisha za ubakaji, kukata shingo Sudan Kusini

Maelezo ya kutisha ya ubakaji, ukataji shingo na mauaji ya risasi nchini Sudan Kusini yameelezwa kwa kina katika ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa juu ya taifa hilo.

Ripoti hiyo inatoa lawama kwa wanajeshi wa serikali na washirika wake.

Mwanamke mmoja, ambaye alisema alipoteza kila kitu aliwaambia wapelelezi kwamba “ingekuwa vizuri kama wangeniua.”

Viongozi walisaini makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Juni yenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ya miaka mitano. Mamilioni wamelazimika kukimbia mapigano hayo.

Maelfu ya watu wameuawa.

Fujo zinazoelezwa kwenye ripoti zinaweza kuwa ni makosa ya kivita na wale waliohusika wanapaswa kufikishwa kwenye mikono ya sheria, tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema.

Jeshi la Sudan Kusini bado halijapokea ripoti hiyo, na hivyo halikuweza kusema lolote, msemaji wake aliliambia shirika la habari la Reuters.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakitazama kipindi cha wiki tano katika miezi ya Aprili na Mei wakati wanajeshi wa serikali na washirika wao waliposhambulia vijiji vinavyoshikiliwa na waasi kusini mwa jimbo la Unity.

Kulitokea mapigano baina ya majeshi ya serikali na waasi, ripoti inasema.

Kwa ujumla, raia 232 waliuawa huku “baadhi wakinyongwa kwenye miti na wengine wakichomwa moto wakiwa hai majumbani kwao,” ripoti hiyo inaongeza.

‘Abakwa huku akitokwa damu baada ya kujifungua

Msichana wa miaka 14 alinukuliwa kwenye ripoti hiyo akisema kwamba hatoweza kamwe kusahamu maovu aliyoshuhudia.

“Nawezaje kusahau kumwona mzee ambaye shingo yake imekatwa kwa kisu kabla ya kuchomwa moto,” alisema.

“Nawezaje kusahau harufu ya miili iliyooza ya wazee na watoto ambao walikuwa wakiliwa na ndege? Hao wanawake ambao walinyongwa na kufa mtini?” msichana aliongeza.

Wachunguzi waligundua kwamba kiasi cha wasichana na wanawake 120 walibakwa na baadhi yao na zaidi ya mwanaume mmoja kwa mara moja (gang-raped), ikiwemo wanawake ambao ndiyo kwanza walikuwa wamejifungua.

“Nilikuwa natokwa damu baada ya kujifungua, lakini askari mmoja alinibaka. Nilikaa kimya na sikumzuia kwani niliona wanawake wengine wakiuawa kwa risasi kwa kukataa kulala na askari na vijana,” mwanamke wa miaka 20 alisema.

Sudan Kusini ilipata uhuru mwaka 2011. Imekuwa ikisumbuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimeshuhudia mauaji ya kimbari na maovu kadhaa, tangu mwaka 2013.

Wanawake mara nyingi wamekuwa wakiandamana kutaka kumalizika kwa mgogoro huo.

Ulianza wakati Rais Salva Kiir alipomfukuza kazi makamu wake Riek Machar, akimshutumu kwa kupanga jaribio la mapinduzi – dai ambalo alilipinga.

Majaribio kadhaa ya kutafuta suluhisho la amani yameshindwa.

Makubaliano ya hivi karibuni, yaliyosainiwa katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yaliwashuhudia viongozi hao wawili wakikubaliana kusitisha mapigano, lakini bado hawajakubaliana juu ya makubaliano ya amani ya kudumu.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.