banner68
banner58

Hakimu alizingatia haya katika uamuzi wake kesi ya Haonga

Hakimu alizingatia haya katika uamuzi wake kesi ya Haonga

11 August 2018 Saturday 09:27
Hakimu alizingatia haya katika uamuzi wake kesi ya Haonga

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, Nemes Chami jana alitumia muda wa saa 1:34 kusoma hukumu ya kesi iliyomuachia huru mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga na wenzake wawili.

Wakati akisoma hukumu hiyo, Hakimu Chami alisema mahakama hiyo ilijiuliza maswali matatu kabla ya kuandika hukumu.

“Mahakama kabla ya kutoa hukumu yake, kwanza ilijiuliza maswali; kwamba ni kweli washtakiwa walitenda kosa? Ushahidi uliotolewa na jamhuri unathibitisha makosa? Na mwisho kama kweli walitenda kosa ni adhabu gani stahiki kwa washtakiwa wote?” alisema hakimu huyo.

Haonga na wenzake, Mashaka Mwampashi na Wilfredy Mwalusanya ambaye ni msaidizi wake walishtakiwa mahakamani hapo kwa makosa ya kusababisha fujo ndani ya chumba cha uchaguzi wa Baraza la Mji mdogo wa Mlowo-Mbozi, kuzuia askari kutekeleza majukumu yao na kukataa amri halali ya kukamatwa na askari.

Washtakiwa hao walidaiwa kutenda kosa hilo Agosti 28, 2017.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Chami alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama hiyo ilijiuliza maswali hayo muhimu.

Alisema baada ya kupitia hoja za upande wa Jamhuri ambao ulikuwa ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Joseph Pande akisaidiana na Baraka Mgaya ambao walikuwa na mashahidi sita, imethibitika washtakiwa wote walikuwepo eneo la tukio lakini mashahidi hao walishindwa kuthitibisha makosa dhidi yao.

“Ukiangalia ushahidi wa shahidi wa nne ambaye ni OCD, na wenzake wengine hakuna mahali panapoonyesha kwamba washtakiwa walikataa kukamatwa,” alisema Hakimu Chami.

“Vile hakuna uthibitisho kwamba washtakiwa waliwazuia askari kutekeleza majukumu yao, hakuna panapoonyesha walikataa kukamatwa wala hakuna mahala panapothibitisha kwamba mshtakiwa wa pili alitaka kurudi ndani ya chumba cha uchaguzi wakati wakiwa nje.”

Hakimu alisema: “Lakini vilevile vifungu vya sheria vilivyotumika na upande wa Jamhuri kuwashtaki washtakiwa hawa havikutakiwa kutumika kulingana na aina ya makosa waliyoshtakiwa nayo.”

Kisha akasema, “hivyo upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha makosa yote ya washtakiwa hawa, hivyo mahakama inawaona hawana hatia na inawaachia huru kuanzia sasa.” Pia hakimu alisema kama kuna upande haukuridhika na hukumu hiyo, wanayo haki ya kukata rufaa ndani ya muda uliowekwa kisheria.

Nje ya Mahakama

Baada ya kumalizika kwa hukumu hiyo, wakili wa Haonga, Boniface Mwakubusi aliwaambia wafuasi waliokuwa nje kwamba mahakama imetenda haki kwa kukubaliana na hoja walizoziwasilisha huku akiwataka kuendelea kuamini kwamba kimbilio pekee lililobaki ni chombo hicho katika kutafuta haki.

“Ninawaambia kwamba tusiogope kudai haki zetu kisheria, sisi sio waalikwa katika hii nchi, hii ni nchi yetu. Wanaweza wakatuleta hapa (mahakamani) lakini hawana uwezo wa kutufunga kila watakapotuleta hapa,” alisema

Katibu mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji alisema, “ni kweli kwamba nchi yetu tumetulia kwa vile tuna imani na mahakama, watendaji waliokadhibiwa kusimamia nchi wamekuwa wakitoa matamko ambayo muda mwingine yanakinzana kabisa na hitaji la sheria na ustawi wa Taifa letu, lakini kwa sababu kuna sehemu wataambiwa ukweli bado tuna imani tumetulia.”

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa alisema wanasiasa hawafanyi kazi ya siasa kwa sababu hawana akili.

“Huyu (Haonga) ni mwalimu kama walimu wengine, angeenda kushika chaki, lakini tunapigwa, tunaonewa, tunanyanyaswa kwa vile tu tunataka Tanzania iwe ni nchi ya kidemokrasia kuwe na utawala bora, kuwe na haki za binadamu na watu wawe na uhuru wa mawazo kujieleza. Hii nchi ni ya sisi sote,” alisema.

Haonga anena

Akizungumza na wapigakura wake, Haonga aliwashukuru kwa uvumilivu na kumtia moyo siku zote za kesi yake huku akiwataka kutorudi nyuma.

“Kesi hii ilinifanya nishindwe kuwawakilisha wananchi wangu vyema bungeni na maeneo yote ya kimaendeleo kutokana na muda mwingi kuiwazia, na mara kwa mara kushinda mahakamani badala ya kufanya kazi nyingine za kuwatumikia,” alisema.

“Lakini tunashukuru Mola leo hii mahakama imetenda haki. Na niwaambie mapambano yanaendelea na sasa wametuongezea nguvu.’’

- Mwananchi

Updated: 11.08.2018 09:31
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.