banner68
banner58

Kauli ya Kangi Lugola kuhusu Gwanda yapingwa, wasomi wamshangaa

Kauli ya Kangi Lugola kuhusu Gwanda yapingwa, wasomi wamshangaa

08 July 2018 Sunday 12:53
Kauli ya Kangi Lugola kuhusu Gwanda yapingwa, wasomi wamshangaa

Siku moja baada ya waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kusema wizara hiyo haihusiki na kutoweka kwa mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Azory Gwanda, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na haki za binadamu wamempinga wakisema anakwepa majukumu yake.

Wachambuzi hao wamesema wizara hiyo inahusika na usalama wa raia na mali zao ikiwamo kutoweka, kutekwa, kuuawa na hata majanga ya asili kama mafuriko.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi wakati wa kikao cha kimkakati cha taasisi za wizara hiyo, Lugola alisema wizara hiyo haihusiki na kupotea kwa Gwanda.

“Zipo hizo habari. Mtu yupo nyumbani kwake halafu ametoweka. Sisi Mambo ya Ndani hatuingilii uhuru wa mtu kutoweka nyumbani kwake. Kila mtu ana uhuru kwa mujibu wa Katiba ya nchi, anaweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuvunja sheria,” alisema Lugola, ambaye ni mbunge wa Mwibara.

Lugola, ambaye amechukua nafasi ya Mwigulu Nchemba aliyeachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri alisema kama Gwanda alitoweka wakati akiwa nyumbani, wao hawahusiki bali wanahusika na mtu aliyetendewa uhalifu ikiwamo kutekwa, akisema katika tukio kama hilo vyombo vya dola humtafuta mtekaji.

Aliongeza, “Hawa ambao wanatoweka kwao tu, wanakuwa na sababu nyingi. Kuna wengine maisha yakiwashinda wanaamua kwenda kwingine.”

Alisema hayo baada ya kuulizwa swali na mwandishi wa habari aliyetaka kujua mkakati wake kuhusu kupotea kwa Gwanda tangu Novemba mwaka jana.

Lugola alisema Wizara ya Mambo ya Ndani haingilii uhuru wa mtu kutoweka akiwa nyumbani kwake.

Maoni ya wadau, wasomi

Akizungumzia kauli ya Lugola, mhadhiri wa masuala ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa (Rucu), Gaudence Mpangala alisema haungi mkono na wala hakutegemea kauli kama hiyo kutoka kwa waziri hasa wa Mambo ya Ndani.

Alisema hakuna mtu anayetoweka kwa hiari yake, huenda ametekwa au ametekwa na kuuawa hivyo ni wajibu wa waziri kufanya utafiti kwanza kabla ya kujibu.

“Pengine kauli yake ingekuwa ni kuwa uchunguzi haukufanywa wa kutosha na sasa ufanyike wa kutosha,” alisema.

Profesa Mpangala alisema wakati ule tukio la Gwanda linatokea, wizara hiyo ndiyo iliyosema inachunguza kuhusu tukio hilo, inakuwaje sasa inasema hawahusiki.

“Watu watekwe, wauawe aseme hahusiki, hiyo ni dalili mbaya. Waziri mpya ajue wajibu wake ni nini, yeye ni mhusika mkuu wa usalama wa watu wake,” alisema.

Profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohammed Bakari alisema, “nadhani waziri hakuwa amefikiria sawasawa, hili suala lilikuwa limeripotiwa polisi, kwa mujibu wa Katiba, wizara hiyo ina wajibu wa kulinda raia.”

Alisema kama tukio limefanyika ndani ya mipaka ya nchi, basi Jeshi la Polisi ambalo kimsingi liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani linatakiwa liwajibike na kama ni nje ya mipaka ya nchi basi polisi wa kimataifa (Interpol), wanahusika. “Inashangaza kuona mtu aliyepita polisi anashindwa kujua sheria, hii ni wizara nyeti, waziri anatoa kauli kama hii kwenye vyombo vya habari, ni hatari,” alisema.

Profesa Bakari alisema waziri mpya wa Mambo ya Ndani anatakiwa ajue kuwa kauli hiyo inavuruga nchi.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema Taifa linapitia kipindi kigumu kwa viongozi kuteuliwa na kufanya kazi sio kwa mujibu wa sheria, bali kwa matakwa. “Kangi ameamua kuliona suala la Azory halina maana kwa sababu aliyemteua hakusema kuwa amemuondoa (waziri wa zamani Mambo ya Ndani), Mwigulu (Nchemba) kwa sababu ya masuala hayo ya kutekwa au kutoweka,” alisema.

Olengurumwa alisema wizara inatakiwa kuangalia usalama wa watu sio tu barabarani, bali hata nyumbani ikiwamo kutekwa au kutoweka. “Changamoto ni moja, waziri anatekeleza aliyoagizwa, ambayo Rais aliyataja kama kipaumbele,” alisema.

Alisema sheria za nchi zinasema Jeshi la Polisi ambalo liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kazi yake ni kulinda watu na mali zao.

“Waziri wa Mambo ya Ndani anaposema si jukumu la wizara, anataka nani afanye hayo?” alihoji na kuongeza:

“Jeshi la Polisi linalinda watu, na sio Azory peke yake, na tayari IGP alikuwa analifanyia kazi, lakini inashangaza kusikia anasema hayo,” alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema Serikali ina wajibu wa kulinda raia wake awe nyumbani, shambani au mahali popote. “Ndiyo maana kukiwa na mafuriko, vitu vya majanga ya asili Serikali inawasaidia kwa sababu Serikali ina wajibu,” alisema.

Msemaji wa Serikali, Hassan Abbasi alisema hawezi kufafanua alichosema Waziri Lugola kwa sababu hakuwepo kwenye tukio na pia hawezi kuzungumzia alichosema waziri.

“Kama mlimuuliza swali halafu akajibu, basi yeye ndiyo amejibu, mimi siwezi kufafanua alichosema waziri,” alisema Abbasi.

Gwanda alitoweka tangu Novemba 21, mwaka jana nyumbani kwake, Kibiti kilomita 130 Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Gwanda ni mmoja wa waandishi wa kwanza kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa serikali za mitaa. Mkewe Anna Pinoni alisema watu wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walimchukua Gwanda kutoka katikati ya mji huo na kutoweka naye.

Mwananchi

Keywords:
KANGI LUGOLA
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.