Maafisa shirika la viwango waleta taharuki kubwa maduka ya Kariakoo

Ukaguzi wa maduka ya vifaa vya umeme jua kuendelea

Maafisa shirika la viwango waleta taharuki kubwa maduka ya Kariakoo

Ukaguzi wa maduka ya vifaa vya umeme jua kuendelea

17 June 2018 Sunday 11:10
Maafisa shirika la viwango waleta taharuki kubwa maduka ya Kariakoo

Na Mwandishi Wetu

WAFANYABIASHARA nchini wameshauriwa kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kuhakikisha wanaingiza, kuzalisha na kuuza bidhaa zenye viwango ili kuepusha madhara kwa watumiaji.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki Kariakoo jijini Dar es Salaam na Ofisa Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Neema Msemwa, wakati wa ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na maofisa wa shirika hilo katika maduka yanayouza vifaa vya umeme wa jua pamoja na kununua sampuli ili kuzipima kwenye maabara za shirika kujiridhisha kama zina viwango vinavyokubalika.

"Nchi hii ni mali yetu wote, hivyo ni lazima kila mmoja wetu awe mzalendo kwa kupenda kuuza na kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora kuepusha madhara kwenye afya zetu," alisema Msemwa.

Aliwataka Wafanyabiashara wa vifaa na umeme wa jua na wengine wote kabla ya kuagiza shehena ya mzigo na kuileta nchini kwa ajili ya kuuzwa wawasiliane na shirika hilo ili wapate ushauri kuhusu viwango vilivyowekwa kwenye mzigo wa bidhaa wanaotaka kuagiza.

Kwa upande wake Mkaguzi wa shirika hilo, Nelson Mugema, alitoa ushauri kwa waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kufuata taratibu zilizowekwa ili kuepuka kuingiza nchini bidhaa hafifu.

Alisema hatua hiyo pia itawasaidia kulinda mitaji yao, kufanyabiashara katika mazingira huru na rafiki na kuepusha madhara kwa nchi yetu.

"Waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi lazima waelewe tukibaini hazikidhi viwango tunaziondoa kwenye soko na wao ndiyo wanaobeba gharama za kuziteketeza au kuzirudisha kule walikozitoa kwa gharama zao," alisema Mugema.

Kwa mujibu wa Mugema, wakaguzi wa shirika hilo wataendelea kufanya ukaguzi kwenye masoko nchini kote ili kununua sampuli za bidhaa mbalimbali na kuzipima ili kuona kama zinakidhi ubora.

Aliwataka wananchi wanapotilia mashaka bidhaa ya aina yoyote kuhusu ubora kwenye soko kuwasiliana na shirika hilo kwa ajili ya hatua zaidi.

Ili kurahisisha majukumu ya kazi yake ikiwemo ukaguzi wa kushtukiza kwenye masoko shirika hilo limefungua ofisi za kanda tano zilizoko kwenye mikoa mitano. Mikoa hiyo na kanda husika kwenye mabano ni Arusha (Kanda ya Kaskazini) Mwanza (Kanda ya Ziwa) Mbeya (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini) Mtwara (Kanda ya Kusini) na Dodoma (Kanda ya Kati).

Azania Post

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.