Makontena 10 ya Makonda yazua utata mpya mnadani

Makontena 10 ya Makonda yazua utata mpya mnadani

02 September 2018 Sunday 13:30
Makontena 10 ya Makonda yazua utata mpya mnadani

Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart ikishindwa kuyauza makontena 20 yaliyoagizwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa mara ya pili, utata umeugubika mnada huo baada ya makontena 10 kutofunguliwa ili wateja kujua bidhaa zilizomo.

Utata huo unakuja wakati tayari Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Rais John Magufuli wakisisitiza makontena hayo kulipiwa kodi, kinyume na Makonda aliyetaka asamehewe kodi kwa kuwa alilenga kuwasaidia walimu wa Dar es Salaam.

Rais John Magufuli alipigilia nyundo makontena hayo kulipiwa kodi baada ya kusema ni mtu mmoja tu nchini mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya wananchi.

Aliyasema hayo Alhamisi iliyopita akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.

“Maana yake si unataka utumie walimu, ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu, ndizo zitapewa mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye shopping mall. Lakini walimu walikwambia wanahitaji makochi, sofa,” alihoji Rais Magufuli.

Katika mnada wa jana ulioanza saa tatu asubuhi, kwenye ghala la Bandari Kavu Dar es Salaam (DICD), makontena 10 yalifunguliwa ili wateja waangalie bidhaa zilizomo, lakini mengine 10 hayakufunguliwa.

Ofisa wa TRA aliyekuwa akisimamia mnada huo na ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema makontena mengine 10 hayakufunguliwa kwa kuwa eneo la ghala hilo ni dogo.

Ofisa huyo alisema wateja walishapewa siku tatu za kukagua bidhaa hizo, hivyo hakukuwa na sababu ya kuyafungua yote.

Kwa upande wake, ofisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) hakuwa na la kujibu.

“Hilo swali muulize mtu wa TRA,” alisema akikataa kujibu wala kutaja jina lake.

Lakini akizungumza na Mwananchi, mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema msimamizi wa mnada ana uhuru wa kuamua bidhaa gani zitangulie kunadiwa.

“Msimamizi wa mnada anao uhuru kuamua kipi kitangulie kuuzwa na kipi kifuatie. Walikuwa na mizigo mingine ya kuuza pia, hivyo huenda walivyofikia 10 wakaamua labda wahamie katika bidhaa nyingine ambazo huenda watu walitaka kununua,” alisema Kayombo.

Mmoja wa wateja aliyejitambulisha kwa jina la Ibrahim Jongo alisema makontena hayo hayakuuzika kwa sababu bei ni kubwa wakati ujazo wake ni mdogo.

“Hata kama ni wewe, uambiwe kontena lile ni Sh10 milioni utatoa au Sh20 milioni? Kwa sababu walivyopakia ni kama wamelundika. Kiutaratibu kwa watu wanaopakia mizigo kwenye kontena wakipanga kiufasaha ni makontena kama sita kati ya 20, itakuwa ni uongo,” alisema Jongo.

Jongo alisema katika siku tano za ukaguzi wa makontena hayo 20, hakuona kontena lenye vitu tofauti bali viti, meza na makabati.

Akifungua mnada huo, mkurugenzi Mtendaji wa Yono Auction Mart, Scholastica Kevela aliwaita waandishi wa habari na kuwaonya kutopiga picha bidhaa zilizomo kwenye makontena hayo wakati wateja wanakagua, jambo lililozidisha utata.

Alitaja masharti mengine kuwa ni wanunuzi kuwa na vitambulisho, leseni za gari na pasi ya kusafiria. Hata hivyo, alisema bado wateja wengi hawajafikia bei zinazotakiwa. Bei zinazotajwa ni kati ya Sh6 milioni hadi 16 milioni.

Akizungumzia mwenendo wa mnada huo, katika ghala la Kurasini Inland Container (KICD), Kevela alisema wamefanikiwa kuuza vifaa 10 katika maghala hayo mawili, lakini wameshindwa kuuza makontena 20 ya Makonda.

“Makontena yalikuwa 20 bei imefika hapo ilipofika na tunaendelea na marketing (uuzaji). Kama ilivyosema Serikali kwamba huu siyo mwisho, nimeeleza tangu mwanzo kila Jumamosi tunafanya mnada, kwa hiyo tutaendelea mpaka makontena yote yapate wateja,” alisema Kevela.

Hata hivyo alisema mnada huo umekuwa na mafanikio kwa kuwa wameuza vifaa 10 yakiwemo magari ingawa siyo makontena ya Makonda.

“Mnada umekuwa very successful (umefanikiwa), tumeuza bidhaa 10, magari na bidhaa nyinginezo. Mnaniuliza makontena mangapi, mimi kwa upande wangu nimeuza kama nilivyopewa maelekezo,” alisema Kevela.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alikataa kutaja bei ya mwisho ya makontena hayo akisema hilo ni jukumu la kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Mwananchi

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.