Rungu la watumishi hewa lahamia CCM

Rungu la watumishi hewa lahamia CCM

08 October 2018 Monday 12:34
Rungu la watumishi hewa  lahamia CCM

Uhakiki uliowafyeka watumishi wa umma, sasa umehamia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Chama hicho tawala kimeanza kufanya uhakiki wa wafanyakazi wake, sawa na ule uliofanywa kwa watumishi wa Serikali tangu mwaka 2016 ambao uliwabaini zaidi ya watumishi hewa 19,000.

Watumishi hao, walibainika baada ya uhakiki huo kufanyika ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Machi 15 mwaka juzi, ili kubaini uwapo wa watumishi hewa ambao baadhi yao waliendelea kulipwa mishahara licha ya kuwa walikuwa wamefariki dunia, kuacha kazi, kustaafu na kufukuzwa.

Rais Magufuli siku hiyo aliwapa wiki mbili wakuu wa mikoa kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa wakiendelea kulipwa mishahara ya Serikali na kutokana na unyeti wa suala hilo haikuwa ajabu kuona akimfukuza kazi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanya Anne Kilango kwa kudai mkoa wake haukuwa na watumishi hewa.

Taarifa ya awali ya watumishi hewa iliyotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilieleza kuwa waligundulika katika mikoa mbalimbali na kuokoa Sh7.5 bilioni, ambazo zingelipwa kama mishahara tangu Januari hadi Aprili 4, 2016.

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kuhusu uhakiki wa watumishi ndani ya CCM na kuthibitishwa na katibu mkuu wake, Dk Bashiru Ally zinaeleza kuwa lengo la uhakiki huo ni kuondoa watumishi hewa ambao chama hicho kinatumia gharama kuwalipa.

Mwananchi limedokezwa kuwa CCM inataka kujua kama inawalipa mishahara watumishi ambao baadhi walikwishafariki dunia, kuacha kazi na wanaofanya kazi nje ya chama hicho.

Uhakiki huo unafanyika kwa watumishi wa CCM waliopo makao makuu, mikoa, wilaya na wanaosimamia vitega uchumi vyake kama viwanja vya mipira.

Pia, uhakiki huo unahusisha watumishi walioko kwenye taasisi zilizo chini ya chama hicho ikiwamo kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL), inayochapisha gazeti la Uhuru, Redio Uhuru na kikundi cha sanaa cha TOT.

Pamoja na mambo mengine, inadaiwa uhakiki huo unakusudia kutambua viwango vya elimu vya watumishi wa CCM ikiwa katika harakati zake za kujifanyia mageuzi na kuwa na watumishi wenye elimu inayoendana na mazingira ya sasa.

Katika kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi mpango huo mtoa habari aliyezungumza na Mwananchi mwezi uliopita limedokezwa: “Kwa mwezi Septemba, mishahara ya watumishi wa chama itapokewa dirishani siyo kutumwa katika akaunti za benki kama ilivyo ada.”

Watumishi wote waliagizwa siku ya kupokea mishahara yao watalazimika kuonyesha picha mbili za pasipoti dirishani zinazomwonyesha mhusika alivyo kwa sasa.

Mwananchi lilipozungumza na Dk Bashiru kuhusu taarifa za uhakiki huo wa watumishi alisema: “Ni kweli tunafanya uhakiki. ‘Human resource audit (uhakiki rasilimali watu) ni jambo la kawaida katika taasisi. “CCM ni chama kikubwa lazima tujue tuna watumishi wangapi ili hata tukitaka kuajiri tujue tunaajiri vipi,” aliongeza.

Alipoulizwa mpaka sasa wamebaini nini, katibu mkuu huyo alisema: “Uhakiki bado unafanyika hadi tupate ripoti tutajua.”

Hata hivyo, Mei Mosi mwaka jana akihutubia kwenye kilele cha sherehe za wafanyakazi mjini Moshi, Kilimanjaro, Rais Magufuli alisema wafanyakazi hewa walioondolewa kwenye mfumo wa malipo ya Serikali ni 19,000.

Akizungumzia uhakiki huo ndani ya CCM, mhadhiri kutoka idara ya sayansi ya siasa na utawala bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema licha ya kuchelewa kufanyika uhakiki huo, itasaidia kuokoa kodi za wananchi kwa njia ya ruzuku.

“Watumishi wa vyama vyote vya siasa wanalipwa kwa kutumia kodi za Watanzania kupitia ruzuku, wanapohakiki maana yake wanajiridhisha na matumizi sahihi ya kodi za wananchi, kwa hiyo jambo hilo limechelewa tu,” alisema Dk Mbunda na kuongeza:

“Tulitegemea CCM ifanye uhakiki kwanza kabla ya kuingia serikalini ili kujitafutia uhalali.”

Dk Mbunda alisema ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha vyama vya siasa kufanya matumizi yasiyoeleweka licha ya ruzuku kutolewa kila mwaka.

Alisema uhakiki huo unatakiwa ufanyike pia kwa vyama vingine vya siasa na kuweka wazi.

Hata hivyo, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema chama chao hakina sababu ya kufanya uhakiki kutokana na idadi ndogo ya wafanyakazi wake.

“Sisi tunafahamiana, hatuna sababu ya kufanya uhakiki, walioajiriwa Chadema kwa ujumla wake ni 82 waliopo makao makuu ya chama Dar es Salaam, ofisi ndogo Zanzibar na kwenye Kanda 10 za chama,” alisema.

Updated: 15.05.2019 10:38
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.