Ubakwaji wanafunzi 17 wa kike Kilimanjaro, waziri atoa tamko

Mengi makubwa yabainika

Ubakwaji wanafunzi 17 wa kike Kilimanjaro, waziri atoa tamko

Mengi makubwa yabainika

08 October 2018 Monday 13:03
Ubakwaji wanafunzi 17 wa kike Kilimanjaro, waziri atoa tamko

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameagiza kufanyika kwa uchunguzi nchi nzima ili kubaini idadi ya wanafunzi wa shule za sekondari waliofanyiwa vitendo vya kifedhuli ikiwemo kulawitiwa.

Waziri Lugola ameenda mbali zaidi na kumwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwaagiza makamanda wa polisi wa mikoa (RPC) kufungua majalada ya uchunguzi katika shule zote.

“Kama wewe unajijua umemfanyia hivyo vitendo mwanafunzi yeyote awe wa msingi au sekondari jipeleke mwenyewe kituoni. Kwa uchunguzi huu tutakufikia tu. Kaa chonjo saa mbaya,” alisema.

Kauli ya Waziri inafuatia taarifa za uwepo wa wanafunzi wa kike 17 wa shule mbili za sekondari wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kudaiwa kubakwa na kulawitiwa wakati wa mkesha wa Mwenge, Septemba 28.

Anayedaiwa kufichua tukio hilo ni mmoja wa wanafunzi anayedaiwa kubakwa siku hiyo na kutupwa kichakani na kupatikana baada ya siku tatu ndipo alipoeleza hakuwa peke yake, bali walikuwa 17.

Baada ya kuhojiwa na kuwataja wanafunzi wenzake wa sekondari za Boma na Hai Day, wanafunzi hao walihojiwa na kukiri kufanyiwa vitendo hivyo mara kwa mara na makundi mbalimbali ya jamii.

Kundi lililotajwa zaidi na wanafunzi hao ni madereva wa pikipiki za biashara maarufu kama “bodaboda”, madereva wa pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) na wauzaji wa santuri au CD.

Tayari watuhumiwa tisa walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Hai Ijumaa iliyopita, huku idadi ya wanafunzi waliobakwa na kulawitiwa ikidaiwa kuongezeka hadi kufikia 19 kutoka 17 ya awali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alinukuliwa na Mwananchi akisema kukamatwa kwa watuhumiwa 12 kulitokana na taarifa alizozitoa mwanafunzi wa sekondari ya Hai.

Alichoagiza Waziri Lugola

Akihojiwa na Mwananchi kwa simu jana kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia uhalifu, Waziri Lugola alisema tukio hilo la wilayani Hai limemfungua macho.

“Kwa maelezo ya wale watoto ambayo nimesoma kwenye gazeti leo (Mwananchi) inaonekana tatizo ni kubwa na si la shule hizo mbili tu, huenda tatizo liko maeneo mbalimbali nchini,” alisema Lugola.

“Inaonekana tatizo ni kubwa. Namuagiza IGP awaelekeze makamanda wa polisi wa mikoa yote nchini kuhakikisha majalada ya uchunguzi yanafunguliwa kila shule wanafunzi wahojiwe,” alisisitiza Waziri.

“Kitendo cha kubaka au kulawiti ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo cha miaka 30. Wahoji kila atakayetajwa awe ni dereva wa bodaboda, teksi, bajaji, mwalimu au yeyote yule akamatwe mara moja.”

“Ninafahamu katika vituo vyetu kuna madawati ya jinsia yanayoshughulika na ukatili wa kijinsia nao washirikishwe wakishirikiana na maofisa wa ustawi wa jamii. Nataka watuhumiwa wote wakamatwe,” alisema.

Waziri Lugola aliwataka wazazi na wanafunzi kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo ili kuwabaini wale wote wanaowatendea wanafunzi vitendo visivyofaa, ili kukomesha tabia hiyo inayokua.

NGO yabaini makubwa zaidi

Mwenyekiti wa taasisi ya Maadili Centre ya Jijini Arusha, Florentine Senya alibainisha kuwa utafiti walioufanya wilaya ya Moshi, umebaini ukubwa wa tatizo la wanafunzi kubakwa na kuingiliwa.

“Wanafunzi wanafanyiwa ukatili wa kingono na baadhi ya ndugu wa karibu, mjomba, kaka, baba wa kufikia. Watoto wanafanyiwa ukatili kuanzia nyumbani, barabarani hadi shuleni,” alisema na kuongeza:

“Hakuna penye afadhali. Wazazi hawahudhurii vikao wala kufuatilia maendeleo ya watoto wao, wala hawajui tabia za watoto wao. Sasa hivi wazazi wengi wanatunza watoto na si kulea watoto”.

“Watoto wameachwa hawana maarifa ya ziada zaidi ya masomo darasani. Kitendo cha wanafunzi wa Hai kimesababishwa na wanafunzi kukosa malezi kuanzia nyumbani na kukosa elimu ya maisha”.

Mwenyekiti huyo alisema pamoja na tatizo kuwa kubwa, bado hakuna mkakati wa dhati wa kukabiliana nalo kwa sababu kipaumbele cha baadhi ya shule ni miundombinu na taaluma na si kulea.

Updated: 15.05.2019 10:38
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.