banner68
banner58

Uraia wa mtu unahusikaje na ‘vinasaba’ vya ukosoaji wa mamlaka?

Uraia wa mtu unahusikaje na ‘vinasaba’ vya ukosoaji wa mamlaka?

11 August 2018 Saturday 11:49
Uraia wa mtu unahusikaje na ‘vinasaba’ vya ukosoaji wa mamlaka?

Suala la uraia limeibuka upya mara hii mwathirika akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze.

Eyakuze alihojiwa na Idara ya Uhamiaji waliotilia shaka uraia wake na hatimaye kumnyang’anya hati ya kusafiria na hata kumzuia kwenda nje ya nchi.

Aidan alinyang’anywa hati yake ya kusafiria Julai 24 na kunyimwa hati ya dharura ya kusafiria na kumsababishia ashindwe kuhudhuria vikao na wadau wa shirika lake katika miji ya Nairobi (Kenya) na Kampala (Uganda). Aidan amesema hana taarifa yoyote ya amri ya kimahakama yenye kuidhinisha hatua hiyo.

Hatua ya kuhojiwa kwa uraia wa Eyakuze inakuja takribani wiki tatu baada ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kuiandikia barua Twaweza ikilitaka shirika hilo kueleza kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yake kwa kile Costech imekieleza kuwa ni kufanya utafiti “usioidhinishwa.”

Utafiti unaozungumziwa na Costech ni ule wa Sauti za Wananchi uliotangazwa mapema mwezi uliopita na Twaweza ambao pamoja na mambo mengine ulionyesha kushuka kwa umaarufu wa Rais John Magufuli.

Utafiti huo uliopewa jina la ‘Si kwa Kwa Kiasi Hicho: Maoni ya Wananchi Kuhusu Siasa’ pamoja na mambo mengine, ulibainisha kuwa umaarufu wa Rais Magufuli umepunguwa kutoka asilimia 71 mwaka jana mpaka asilimia 55 mwaka huu.

Baada ya siku chache Costech kushindwa kueleza ni kwa sheria ipi walikusudia kuiadhibu Twaweza, wakala huyo anayehusika na masuala ya tafiti za kisayansi nchini alinukuliwa akisema kwamba Twaweza walishaijibu barua yake (Costech) kwa wakati na kwamba hakuna hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya shirika hilo (Twaweza) linalojihusisha na ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu masuala mbalimbali.

‘Hatuendeshwi na siasa’

Suala la kuhojiwa kwa uraia wa Eyakuze ambalo bado linaendelea kurindima nchini limeibua maswali mengi zaidi kuliko majibu, moja likiwa ni kwa nini mara zote uraia wa wale wanaoonekana kuikosoa Serikali huhojiwa?

Ni bahati nzuri kwamba msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda ameshawahi kulipatia majibu swali hili, jibu ambalo hata hivyo wengi wanaliona ni la kijujuu na halikati kiu.

Mtanda ambaye anakiri idara hiyo kuishikilia hati ya kusafiria ya Eyakuze na kumzuia kusafiri nje ya nchi, anasema kwamba shughuli za ofisi yake haziendeshwi kisiasa kama vile baadhi ya watu wanavyodai.

Anafafanua: “Ikiwa wasiwasi juu ya uraia wa mtu fulani unaibuka sisi huwa tunafanya kazi yetu ili kujiridhisha na kuondoa huo wasiwasi.”

Lakini, Mtanda anakwepa kuzungumzia swali ambalo ndio kiini haswa la jambo lenyewe: kwa nini wanaoonekana kuwa wakosoaji uraia wao uhojiwa?

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi anajaribu kulipatia majibu swali hili, akisema kwamba kesi ya Eyakuze inashughulikiwa kama ya mtu mwingine yeyote. “Hii ndio tunaita utawala wa sheria,” anafafanua.

“Haki za Eyakuze hazijakiukwa, na hana hatia mpaka pale atakapokutwa nayo kwa mujibu wa sheria za nchi.”

Si kipya, ni desturi

Uzoefu, hata hivyo, unatuonesha kwamba kuhojiwa kwa uraia wa Eyakuze si kitu kipya nchini bali ni mwendelezo tu wa kile ambacho sasa kimekuwa ni desturi ambapo watu ambao wanaonekana kuthubutu kuibua maswali magumu dhidi ya Serikali wamekuwa wakijikuta uraia wao ukitiliwa shaka.

Huu ndio msingi wa maoni ya wengi—wale ambao hukabiliana na usumbufu huo na wale wanaowaonea huruma—kwamba lengo ni kuwanyamazisha wanaohoji na kuwatisha wale wanaopanga kufuata nyao zao.

Mfano wa hivi karibuni na ambao kesi yake bado inaendelea ni ule wa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSN) na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo ambaye mpaka muda huu uhamiaji hawanajamwambia kama ni raia au hapana.

Nondo alishutumiwa kwa “kujiteka” na mpaka wakati wa kuandika makala haya, kijana huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za wanafunzi, amesimamishwa masomo ili kesi yake inayoendelea mahakamani imalizike.

Nondo iliyomkosa Mwigulu

Pamoja na mambo mengine, Nondo aliwahi kumtaka aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kujiuzulu kutokana kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwilini baada ya kupigwa risasi wakati jeshi la polisi likiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wafuasi hao walikuwa wanatembea kuelekea ofisi za Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kumshinikiza atoe hati za kiapo kwa wasimamizi wa Chadema wakati wa uchaguzi mdogo wa Kinondoni. Katika kuwatawanya wafuasi hao maeneo ya Mkwajuni, Kiondoni, ambapo moja ya risasi ilimpiga Akwilina akiwa kwenye daladala.

Mtu mwingine ambaye uraia wake uliwahi kuhojiwa ni Mratibu wa Muungano wa Walinzi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa ambaye alihojiwa Julai 24 mwaka jana na maofisa uhamiaji waliovamia ofisini kwake.

Hawakumueleza sababu za kumuhoji badala yake walimwambia kuwa lilikuwa ni agizo “kutoka juu.” Olengurumwa alidai kuwa kuhojiwa kwake kumechangiwa na harakati zake za kupigania haki za ardhi za jamii ya Kimasai katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Ripoti zilikuwa zikionyesha wakati huo kwamba jumla ya nyumba 100 za Wamasai zilichomwa moto huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikidaiwa kuhusika.

Siku ambayo maofisa wa uhamiaji walienda kumuhoji Olengurumwa kwa mara ya kwanza, THRDC ndio kwanza walikuwa wametoka kutoa tamko la kulaani kile ilichokielezea kama “dhuluma inayofanywa na serikali dhidi ya jamii ya Wamasai.”

“Lengo lao ni kuvuruga mapambano yetu (dhidi ya dhuluma) dhidi ya wanakijiji hawa wasio na msaada kwa kusema kwamba wale wote wanaowapigania (wanakijiji hawa) ni Wakenya,” anateta Olengurumwa.

Ulimwengu na ya ulimwenguni

Pengine tukio lililomo katika kumbukumbu za walio wengi ni lile la Februari 12, 2002 ambapo serikali ya awamu ya tatu ilimtaka mwanahabari nguli Jenerali Ulimwengu kuthbitisha uraia wake.

Hili lilianza mapema Februari 2001 ambapo serikali ilimkana Ulimwengu kuwa siyo raia wa Tanzania. Uamuzi huu uliwashtua wengi ndani na nje ya nchi ikizingatiwa kuwa Ulimwengu amekuwa sauti muhimu katika uwanja wa asasi za kiraia nchini na ulimwenguni kwa ujumla. Pia, amewahi kutumikia nafasi mbambali za uongozi kama vile mbunge na mkuu wa wilaya.

Ulimwengu kama ilivyo kwa wengine, hakuwahi kupewa sababu za kunyimwa uraia wa taifa pekee analolijua, Tanzania.

Katika mahojiano yake aliyowahi kufanya na Shirika la Habari la Ujerumani (DW) mwaka 2010, Ulimwengu alisema kwamba mara nyingi suala la uraia huletwa na watu wasio kuwa na nia njema. Yeye anaamini kwamba haingii akilini kutishia kumpokonya mtu uraia wake eti kwa kuwa tu hukubaliani naye katika vitu fulani.

“Kwa upande wangu ilikuwa ni wazi kabisa kwamba watawala walitaka nishike adabu yangu na walipodhani nimeshaingia adabu rais aliwaambia watu wake wanipatie uraia.” Ulimwengu anajulikana kwa makala zake alizokua akiandika na kuchapishwa na gazeti la RAI.

Bashe naye aliambiwa basi

Lakini, kama utadhani kwamba ni uraia wa wakosoaji tu unaohojiwa basi utakuwa umekosea kwani hata kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alishawahi kuambiwa siyo raia, cha kushangaza hili lilifanywa na wapinzani wake ndani ya chama. Mnamo mwaka 2010 kuelekea Uchaguzi Mkuu, Kamati Kuu (CC) ya CCM ilimwengua mbunge wa sasa wa Nzega Mjini, Hussein Bashe katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo kwa madai ya kuwa uraia wake ulikuwa na mashaka.

Bashe aligombea katika kura za maoni katika jimbo hilo na kumshinda Lucas Selelii ambaye alikuwa akitetea kiti chake. Hata hivyo, serikali baadaye ilimtangaza Bashe kuwa raia halali wa Tanzania na sasa ni mbunge.

Mwaka 2014, wakili wa Mahakama Kuu, Alberto Msando alihojiwa uhalali wa uraia wake na maofisa wa Uhamiaji kutoka Mkoa wa Kilimanjaro waliokuwa wakitilia shaka uraia wake.

Wakati huo Msando alikuwa anamtetea mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe katika kesi yake dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mwaka jana tu Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi naye pia alihojiwa juu ya uhalali wa uraia wake punde tu baada ya kumtaka Rais Magufuli afufue mchakato wa kuandika Katiba Mpya wakati wa mkutano na asasi za kiraia.

Askofu Niwemugizi alitonesha kidonda wakati ambao Rais ameshaweka wazi msimamo wake kwamba Katiba Mpya si moja kati ya vipaumbele vya Serikali yake.

Uraia na utafiti?

Suala la kuhojiwa uraia wa Eyakuze limewashangaza wengi, mmoja wao akiwa ni Padre Privatus Karugendo ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter ameshindwa kuona uhusiano kati ya kazi inayofanywa na Twaweza na kuhojiwa kwa uraia wa mkurugenzi mkuu wake. Anauliza:

“Siwatetei Twaweza, inawezekana wamefanya makosa. Hoja yangu ni, makosa hayo yana uhusiano gani na hati ya kusafiria ya Aidan Eyakuze?”

Suala la Eyakuze pia lilikiibua Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho punde tu baada ya habari hizo kuenea kituo hicho kilitoa tamko kikalaani hatua hiyo ya Serikali na kuitaka iheshimu haki za binadamu ikiwamo ile ya raia kuwa huru kutembea kutoka eneo moja hadi jingine ndani ya nchi.

“Tuna taarifa kwamba hati ya kusafiria ya Aidan Eyakuze inashikiliwa bila ya kupewa sababu zozote,” imesema LHRC katika tamko lake. “Tunalaani vikali kitendo hicho.”

Kuna watu wameelezea hatua ya Serikali kuhoji uraia wa watu kama “unyanyasaji.” Nilimuuliza wakili wa Mahakama Kuu, Jebra Kambole ni nini haswa kinapaswa kuitwa unyanyasaji?

Alichosema ni kwamba wao kama wanasheria hukielezea kitu kama “unyanyasaji” kutegemea ni mara ngapi kinafanyika na muda kinaochukua.

“Tunategemea kuwa baada ya mtu kuhojiwa uraia wake atapatiwa mrejesho wa matokeo bila muda kuchelewa,” hivyo ndivyo ilivyo kwa mujibu wa Kambole. “(Kwani) hii humsaidia mtu kuondokana na msongo wa mawazo unaoweza kusababishwa na kutokujua nini kitafuata baada ya uchunguzi.”

Anaonya kwamba hii haikusudii kuwazuia Uhamiaji kufanya kazi yao kwa mtu ambaye uraia wake wanautilia mashaka. “Lakini wanahoji katika mazingira gani? Mara ngapi na huchukua muda gani?”

Hata wewe unaweza kuhojiwa

Vyovyote itakavyokuwa, Mtanda, msemaji wa Uhamiaji, ameendelea kusisitiza kwamba wao wanafanya kazi zao na wala hawakusudii kumnyanyasa mtu.

“Tunawahoji watu uraia wao kuzingatia taarifa tunazozipata kutoka kwa raia wema,” anasisitiza Mtanda. “Tukipata taarifa zinazotilia shaka, kuhusu uraia wako (wewe mwandishi) basi lazima utahojiwa.”

Khalifa Said ni mwandishi wa habari Simu: +255 716 874 501; Email: khalifaxsayed@gmail.com

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.