Wabunge wapokea bajeti kwa hisia tofauti

Wabunge wapokea bajeti kwa hisia tofauti

15 June 2018 Friday 18:12
Wabunge wapokea bajeti kwa hisia tofauti

Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 ya Sh32.4 trilioni iliyowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango imepokewa kwa hisia tofauti na wabunge.

Wakizungumza na Mwananchi katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana, baadhi wameipongeza Serikali kwa kufuta kodi na tozo kadhaa.

Lakini Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema hofu yao kubwa katika bajeti hiyo ni ongezeko la Deni la Taifa ambalo haliendani na makusanyo ya mapato.

Mbowe, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, alisema yapo mambo ya msingi katika mapendekezo ya bajeti ambayo yanatia moyo, kama kupunguza makali ya kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Wakati Mbowe akionyesha hofu hiyo, mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye na Hussein Bashe (Nzega Mjini-CCM) wamepongeza bajeti wakisema inatoa mwanga kwa wananchi.

“Hii ni bajeti bora kabisa kuwahi kusomwa na Waziri Mpango. Imeonyesha njia katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo,” alisema Bashe.

“Ziko hatua zimechukuliwa kwa kulinda viwanda vyetu vya ndani. Ni hatua nzuri ambazo zikitekelezwa zitakuwa na tija na hasa kusaidia katika uwekezaji wa sekta binafsi.”

Lakini Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee alisema “bajeti hiyo ni hewa” kama ilivyokuwa kwa bajeti ya mwaka uliopita.

“Hakuna miujiza katika ukusanyaji wa mapato. Tatizo kubwa ni katika utekelezaji. Mwaka 2017/18 bajeti ilikuwa Sh31 trilioni lakini ni Sh21 trilioni tu ndizo zilizokusanywa,” alisema Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe (Chadema).

Alisema katika mapendekezo ya bajeti, miongoni mwa vipaumbele ni kilimo na viwanda lakini bajeti za wizara hizo, hasa kwa upande wa miradi ya maendeleo, zimepungua.

Mdee alisema hivi karibuni Bunge lilitoa ripoti kuhusu uvuvi wa bahari kuu jinsi mapato yanavyopotea, lakini katika mapendekezo hayo hakuna eneo lililogusa uvuvi wa bahari kuu.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema: “Bajeti hii haina tofauti na ile ya mwaka jana kwa wananchi wa kawaida, kodi ambazo alipandishiwa mwananchi wa kawaida hazijashushwa.”

Zitto, ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, alisema kupunguza kodi kunatoa ahueni kwa Serikali na wafanyabiashara, lakini wananchi wa kawaida wataendelea na maisha yaleyale.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema: “Tangu tumepata uhuru bajeti yetu imekuwa inategemea maeneo yaleyale ya kodi, bia, soda, juisi, sigara. Mpaka leo ni yaleyale.”

Wabunge wengine waliozungumza Abdallah Bulembo (Kuteuliwa -CCM); Stanslaus Mabula (Nyamagana -CCM); Livingstone Lusinde (Mtera -CCM) na Margaret Sitta (Urambo -CCM) walisema bajeti ni nzuri kwa sababu imelenga kulinda viwanda vya nchini.

“Taulo za kike bei yake imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake, kuondolewa kwa kodi kutawawezesha wanawake na wanafunzi wa kike wanaotoka familia masikini kumudu, kuzinunua,” alisema.

Updated: 15.06.2018 18:28
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.