Wamiliki blogu Tanzania washindwa masharti TCRA

DarMpya, Makonda Media na nyingine ni miongoni mwa zilizofungwa

Wamiliki blogu Tanzania washindwa masharti TCRA

DarMpya, Makonda Media na nyingine ni miongoni mwa zilizofungwa

15 June 2018 Friday 17:57
Wamiliki blogu Tanzania washindwa masharti TCRA

Siku chache baada ya mtandao wa Jamii Forums kusitisha huduma zake hewani, hali kama hiyo imejitokeza pia kwa mitandao mingine ya kijamii ikiwamo blogu ambazo zimetangaza kutokuwa hewani kutokana na kile kilichoelezwa ni kushindwa kufikia vigezo vilivyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Miongoni mwa mitandao hiyo iliyotoa taarifa ya kusitisha huduma zake ni pamoja na Darmpya blogu, Makonda Media na Innowisetz.

Kuanzia Juni 14 mwaka huu, vyombo vya habari vya mitandaoni kama vile blogu, redio pamoja na televisheni zinazoruka kupitia chaneli ya you tube zinatakiwa kusajiliwa na TCRA na kisha kupata kibali cha kuendelea kutoa huduma.

Tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge mapema mwaka huu kumeshuhudiwa mitandao mingi ikiwamo ile iliyokuwa na wafuasi wengi ikisitisha shughuli zao.

Kwa mujibu wa TCRA, waombaji wanaotaka kusajili blogi wanapaswa kulipa Sh100,000 kama gharama ya fomu na baadaye kutakiwa kulipa Sh1,000,000 kama ada kwa ajili ya kupata leseni.

Hatua hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu iliyofanya blogu nyingi kulazimika kufunga shughuli zao kutokana na kushindwa kumudu gharama hizo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, mmiliki wa blogu ya Darmpya, John Marwa amesema TCRA ilipaswa kutoa notisi ya angalau mwaka mmoja kukamilisha masharti hayo na siyo ilivyo sasa ya kutaka kukamilisha matakwa hayo ndani ya wiki tatu.

“Hatuko kinyume na matakwa ya TCRA lakini masharti hayo yametolewa ghafla mno na imekuwa changamoto kubwa kwa baadhi yetu ambao ndiyo kwanza tumeingia kwenye tasnia hii,” alisema.

Kwa upande wake Mohamed Ramadhani wa Makonda Media amesema kukua kwa teknolojia ndiyo sababu iliyowasukuma vijana wengi kuingia kwenye uwanja huo wa kuendesha mitandao ya kijamii.

“Teknolojia ndiyo sababu kubwa ambayo imetusukuma vijana wengi kuingia kwenye jukwaa hili lakini tumelazimika kusitisha huduma zetu kutokana na notisi ya ghafla kutoka TCRA,” amesema.

Hata hivyo, kaimu meneja uhusiano wa TCRA alikanusha madai hayo akisema sheria inasema watoaji huduma za maudhui kwenye mitandao wanapaswa kusajiliwa na hakuna muda utakaoongezwa.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.