Ubabe wa Rais Donald Trump waleta sintofahamu kwenye Umoja wa Mataifa

Aonyesha ubabe, kutojali mataifa mengine

Ubabe wa Rais Donald Trump waleta sintofahamu kwenye Umoja wa Mataifa

Aonyesha ubabe, kutojali mataifa mengine

03 October 2018 Wednesday 08:38
Ubabe wa Rais Donald Trump waleta sintofahamu kwenye Umoja wa Mataifa

“Tunakataa itikadi ya dunia kijiji kimoja, tunakumbatia kanuni ya uzalendo.” Ni kauli ya kibabe ya Rais wa Marekani, Donald Trump kwenye mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huku akisisitiza Marekani itafanya jambo kwa masilahi yake.

Kama hiyo haitoshi, Trump anajigamba kuwa Marekani imejitoa kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na haitarudi, pia haiungi mkono wala kuitambua Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Wakati Trump akionyesha msuli kwa viongozi wenzake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kama vile alijua kutakuwa na hotuba za kibabe alijielekeza zaidi kuwasihi wajumbe wa mkutano huo akisema, “Dunia inaumwa ugonjwa wa kukosa uaminifu wa kudhibiti matatizo.”

Lakini, serikali ya China katika mkutano huo iliamua kuwapa wajumbe maswali magumu kwamba “Je, tuendelee kuwa na mshikamano au tuuvuruge? Je, tunahitaji kuendelea kuheshimu taratibu tulizojiwekea au tuziache zivurugike?

Mbali na hao Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu, María Fernanda Espinosa Garcésa mbaye pia ni balozi wa Ecuador alijumlisha hoja hizo na zingine zilizotolewa na viongozi wengine wa serikali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwamba “mshikamano katika kushughulikia tatizo kwa pamoja ndio njia pekee ya kukabiliana na changamoto za dunia.”

Anasema dunia imekumbwa na machafuko, vita na athari za mabadiliko ya tabianchi. Rais huyo, huku akitumia msemo wa wahenga wa nchi yake, anawataka viongozi kutumia kanuni ya kukabiliana na matatizo inayoitwa ‘Minga’. Kanuni hii inahimiza ushirikiano katika kushughulikia jambo kwa faida ya wananchi.

Rais huyo anasema ili kukabiliana na matatizo na changamoto zingine za dunia, wanapaswa kuunda ‘kijiji cha ushirikiano’ au ‘globalminga’. Kwa maana ushirikiano wa kidunia katika kuijenga jamii itakayoishi kwa amani na utulivu.

Mshikamano

Katika kuonyesha kwamba mshikamano ndiyo dawa ya kupambana na karaha za dunia, Katibu mkuu wa UN, Guterres hakuwa mbali na rais wengine, anaposema mshikamano unaohitajika sasa kutatua matatizo ya dunia hivi sasa uko chumba cha wagonjwa mahututi.

Katibu mkuu, María Fernanda anamnukuu mtaalamu wa sayansi ya siasa, Graham Allison kwenye kitabu chake ‘Destined for war’ kwa maana ya kukusudia vita kwamba iwapo viongozi watawajibika kuweka mikakati ya ushirikiano katika kudhibiti maslahi ya kiushindani, inawezekana kuepuka vita na kuifanya dunia kuwa sehemu salama.

Hotuba nyingi za viongozi zilitawala neno la Kiingereza ‘multilateralism’ kwa maana kuwa, walau nchi tatu au zaidi zinaweza kushirikiana kutatua tatizo fulani katika dunia.

Wengine waliongeza neno ‘unilateralism’ kwa maana ya taifa moja linapojiamulia kushughulikia tatizo la kidunia bila kushirikisha nchi nyingine. Mfano, mwaka 2003 Marekani ilipoamua kuivamia kijeshi Iraki haikuungwa mkono na taifa lolote.

Katibu mkuu, Guterres katika kauli yake ya dunia inaumwa ugonjwa wa kukosa uaminifu wa kudhibiti matatizo, anasema uaminifu kwa watu wengine duniani umefika kikomo, wengi wanahisi hawako salama kwa maana uaminifu katika taasisi za serikali haupo na uaminifu kati ya nchi na nchi ni mdogo.

Pia, uaminifu katika kufuata sheria za kimataifa ni duni, ndani ya nchi zenyewe watu wametokwa imani na masuala ya kisiasa, utawala wa sheria haupo na ndani ya Baraza la Usalama la UN kumekuwa na mgawanyiko mkubwa.

Guterres anatoa mfano wa nchi za Ulaya enzi hizo kwamba ukosefu wa utatuzi wa matatizo kwa kushirikiana ndio uliosababisha kuzuka kwa vita vya dunia, vile vya kwanza hadi vya pili na kusababisha kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 1945 ambayo sasa inaitwa Umoja wa Mataifa.

Anasema kuna haja ndani ya Umoja wa Mataifa kuonyesha thamani ya ushirikiano wa kimataifa kwa kuleta amani, kutetea haki za binadamu na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi.

Guterres anasema mwaka jana alipohutubia kwenye mkutano wa 72 aliainisha changamoto saba, lakini zote hadi sasa hazijapata ufumbuzi ikiwamo kushindwa kumaliza vita Syria, Yemen na maeneo mengine duniani.

Anasema changamoto zingine wananchi wa Rohingya bado wanaishi uhamishoni, Palestina na Israel bado wako kwenye mgogoro usioonekana mwisho wake, ugaidi na matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya hazijapata ufumbuzi.

Katibu mkuu amewaambia viongozi hao kwamba mwaka huu dunia inaadhimisha mwaka wa 70 tangu kutolewa tangazo la la Haki za Binadamu, lakini ajenda hiyo imeonekana kupuuzwa na hasa na mataifa makubwa kama Marekani.

Anasema dunia sasa imetawaliwa na siasa za kuona kila kitu kibaya, hali inayotishia usalama kwa wananchi wengi.

China na busara zake

Licha ya China kutoa swali gumu kuhusu umuhimu wa mshikamano na kuheshimu taratibu, pia iliweka hadharani jibu la swali hilo kwamba nchi hiyo itaendelea kuheshimu na kuzitekeleza taratibu zilizowekwa katika kuendeleza mshikamano duniani.

Hotuba hiyo iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni, Wang Yi iliweka wazi kwamba nchi hiyo inaamini changamoto za dunia zitatatuliwa kwa ushirikiano na hakuna nchi inayoweza kuzitatua pekee yake.

Anasema China inaamini maendeleo yatapatikana kwa kushirikiana badala ya kutaka kuonekana mshindi kwa kutaka kufanya kila kitu mwenyewe. Na kwamba ushirikiano wowote lazima uwe na mwongozo na siyo wa msukumo.

Pia, ilisisitiza umuhimu wa haki na usawa katika masuala ya kimataifa bila kujali udogo wa nchi au umasikini wake.

Ubabe wa Trump

Pamoja na kwamba Marekani inaamini zaidi katika ubabe, hotuba ya Trump kwenye mkutano huo iliheshimu mshikamano ulioonyeshwa na nchi za China, Japan na Korea Kusini katika kushughulikia tishio la makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini.

Trump aliueleza mkutano huo mafanikio ya mkutano wake na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un uliofanyika Juni nchini Singapore kwamba tangu wakati huo hakuna tena majaribio ya makombora wala vitisho vya nyuklia.

Ukiacha eneo hilo, sehemu kubwa ya hotuba ya Trump ilikuwa ni ubabe na majigambo ya namna alivyoleta mafanikio na matumaini mapya kwa wananchi wa Marekani kuliko marais waliomtangulia.

Aliishambulia serikali ya Iran kwamba imeshindwa kutekeleza makubaliano ya kuachana na mpango wake wa nyuklia, na kueleza kwamba mwaka 2015 Marekani iliamua kujitoa kwenye mazungumzo ya nyuklia na Iran na Agosti iliiwekea vikwazo nchi hiyo na vingine vitaongezwa Oktoba.

Trump alijigamba kwamba siku zote Marekani itafanya jambo kwa masilahi yake, huku akisema mwaka jana kwenye mkutano kama huo alieleza matatizo yaliyomo ndani ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kutaka lifumuliwe.

Aliwaeleza wajumbe kuwa Marekani iliamua kujitoa kwenye baraza hilo na haitarudi hadi lirekebishwe kwa kuwa limekuwa likiwalinda wavunjaji wa haki za binadamu. Pia, alisema kwa sababu hizo hizo Marekani haitaunga mkono wala kuitambua ICC, huku akiishambulia kuwa haina hadhi wala mamlaka na imevunja kanuni zote za haki za binadamu.

Jeuri ya Trump ilikwenda mbali zaidi aliposema Marekani imekataa itikadi ya dunia kijiji kimoja na kwamba wao wanakumbatia kanuni za uzalendo, kwa maana taifa lenye kuwajibika lazima lijilinde na hatari yeyote.

Aliendelea kumuonyesha ubabe Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kwa kumtangazia vikwazo zaidi na washauri wake wa karibu, lakini pia akajigamba ameongeza bajeti ya jeshi kwamba mwaka huu ametoa dola 700 bilioni na mwakani ataongeza zifike dola716 bilioni na kulifanya jeshi la Marekani liwe lenye nguvu duniani.

Trump pia aliiponda Venezuela kwamba ni taifa tajiri, lakini limekuwa masikini kwa kuendekeza siasa za ujamaa uliosababisha rushwa, ufujaji wa mali za umma hali iliyosababisha wananchi wawe wakimbizi.

Kiongozi huyo wa 44 wa Marekani, taifa linalofuata mfumo wa kibepari, aliuponda mfumo wa siasa za kijamaa na kikomunisti waziwazi na kuzitaka nchi wanachama wa UN kuukata mfumo huo kwa kuwa unasababisha matatizo kwa wananchi.

Alijigamba Marekani ndio taifa pekee duniani lenye kutoa misaada mingi lakini halinufaiki chochote na alitahadharisha kuwa kuanzia sasa wataanza kufanya tathmini ya misaada wanayotoa kwa kuzipima nchi zinazonufaika kama zinaipenda Marekani kwa dhati.

Trump anasisitiza kwamba wataanza kutoa misaada kwa nchi zinazowaheshimu na ambao ni marafiki wa kweli, huku akisisitiza kwamba hata uchangiaji wao katika Umoja wa Mataifa hautazidi asilimia 25 ya bajeti ya walinda amani wa umoja huo, lengo ni kuzifanya nchi nyingine zichangie.

Alimsifu Mfalme Salman wa Saudi Arabia kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuleta mbadiliko katika taifa hilo la Kiarabu.

Kenyatta na fedha haramu

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika hotuba yake iligusia kwa karibu hoja za katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres kuhusu tatizo la ukosefu wa uaminifu linavyozidi kuongeza pengo kati ya wananchi na taasisi za serikali duniani.

Uhuru bila kumung’uny’a maneno alisema pamoja na kwamba viongozi wengi hasa wa nchi zinazoendelea wanataka mabadiliko katika Umoja wa Mataifa, lakini wajue hitaji muhimu na linalosababisha pengo kati ya wananchi na serikali ni uwajibikaji duni, hali hii inasababisha rushwa na upotevu wa rasilimali za umma.

Aliyashambulia mataifa makubwa bila kuyataja majina kwamba yanashiriki mtandao wa usafirishaji wa fedha haramu, kutokana na kushindwa kuchukua hatua za makusudi za kupambana nao.

Uhuru ameyasema hayo kwenye Umoja wa Mataifa wenye nchi wanachama 193 kwamba yanayotokea Afrika ndiyo yanatokea katika mataifa mengine. Anatoa takwimu kwamba kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 2009 fedha haramu zilitoroshwa ni kati ya dola 1.2 trilioni na dola 1.4 trilioni.

Uhuru alibainisha mbele ya wajumbe wa mkutano huo ambao ni viongozi wa nchi na serikali kwamba mfumo wa utoroshaji fedha haramu ndio mfumo unaotumiwa na mtandao wa dawa za kulevya na mtandao wa ugaidi.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.