UN yatoa nafasi ya mwisho kwa vikundi vinavyozozana Sudan Kusini

UN yatoa nafasi ya mwisho kwa vikundi vinavyozozana Sudan Kusini

01 June 2018 Friday 17:46
UN yatoa nafasi ya mwisho kwa vikundi vinavyozozana Sudan Kusini

PANDE mbili zinazozozana huko Sudan Kusini zimepewa nafasi ya mwisho kufikia makubaliano vinginevyo vijiandae kwa vikwazo vikali.

Tayari Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezipa pande hasimu nchini humo muda wa mwezi mmoja kufikia makubaliano ya amani la sivyo wawekewe vikwazo.

Mswada wa azimio hilo ulioandaliwa na Marekani, ulipata ushindi mdogo wa kura 9 katika baraza hilo lenye nchi wanachama 15.

Nchi 6 zikiwemo China, Urusi na Ethiopia ambazo ni washirika muhimu katika juhudi za kutafuta amani ya eneo hilo hazikupiga kura.

Azimio hilo linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kuwasilisha ripoti ifikapo Juni 30, kueleza ikiwa makubaliano yaliofikiwa mwezi Disemba yanatekelezwa na ikiwa pande husika zimepata suluhisho muafaka la kisiasa kusitisha mapigano.

Ikiwa makubaliano hayo ambayo ndiyo ya karibuni zaidi miongoni mwa mkururo wa makubaliano yaliyofikiwa hayatakuwa yametekelezwa, basi baraza hilo la usalama litamuwekea vikwazo waziri wa ulinzi wa Sudan Kusini pamoja na maafisa wengine watano na pia uwezekano wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kuuziwa silaha.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameliambia baraza hilo kuwa Marekani imepoteza subira.

"Marekani imepoteza subira yake. Hali iliyoko kwa sasa haikubaliki. Wakati umewadia wa sisi sote kudai hali nzuri kwa raia wa Sudan Kusini."

Azania Post

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.