Mhadhiri IFM:Nidhamu, kujituma ndio urithi sahihi kwa watoto

Mhadhiri IFM:Nidhamu, kujituma ndio urithi sahihi kwa watoto

15 September 2019 Sunday 17:41
Mhadhiri IFM:Nidhamu, kujituma ndio urithi sahihi kwa watoto

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

MHADHIRI wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk Indiael Kaaya amesema nidhamu na kujituma ndio urithi sahihi unaotakiwa kurithishwa kwa watoto.

Amesema hata mtoto akizaliwa katika familia yenye kila kitu, akikosa nidhamu na kujituma ni ngumu kufanikiwa katika maisha

Amesema hayo leo Septemba 15, 2019 katika mahafali ya tano kwenye shule ya msingi  New Version Nursary & Primary School iliyopo Kibaha kwa Mathiasi eneo la Msangani.

“Natamani watoto wajue hakuna mbadala wa kujituma na kuwa na nidhamu kwa sababu kila aliyefanikiwa katika maisha kuna wakati alijituma na kujinyima hivyo ukipata nafasi ya kufanya kitu iwe shule ama ofisini fanya kwa ufanisi na bidii yako yote na nidhamu ya kujua unachotaka kukifanya ukifanye kwa wakati gani,” amesema Dk Kaaya.

Amesema maisha ya sasa yanamabadiliko mengi na ushindani unaongezeka hasa katika kipindi hiki cha mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo teknolojia imechukua nafasi kubwa.

‘‘Wazazi, walimu wanatakiwa kuwasaidia watoto kutumia vipaji vyao, wengi waliofanikiwa na kufikia malengo ni ambao wanachanganya elimu waliyonayo na vipaji vyao. Ukiona mtoto wako anapenda kufanya kitu fulani ikiwemo kupika mpe fursa na umtengenezee mazingira ambayo yatamfanya asipate madhara,’’ amesema.

Vile vile Dk Indiael amewataka wazazi kuwawekea watoto mipaka ya matumizi ya simu ili wasipoteze ufanisi katika shughuli zao za kila siku.

Mkuu wa Shule hiyo, Zulfa Lema amesema shule hiyo imeshika nafasi ya tatu kiwilaya na mkoa wa Pwani na mwaka 2017 ilishika nafasi ya 96 kitaifa na mwaka 2018 ilishika nafasi ya 175 kitaifa.

“Malengo tuliyojiwekea si kufaulisha watoto tu bali kuhakikisha vijana wetu wanapata nafasi katika shule za watoto wenye vipaji maalum jambo ambalo limekuwa likitokea mwaka hadi mwaka,’’ amesema na kuongeza

“Kutokana na mwendelezo wa matokeo mazuri mwaka 2017 waziri wa elimu Profesa Joyce Ndalichako alitutunuku cheti ikiwa ni shule ya msingi bora kitaifa miongoni mwa shule ya mtu binafsi,’’

Meneja wa Shule hiyo, Magreth Moshi amesema watoto waliosoma shuleni hapo wamefunzwa kufanya kazi na watakapokuwa majumbani wazazi wahakikishe wanawaendeleza.

PICHANI:Mkurugenzi wa shule ya msingi  New Version, Andrew Madunda akimpongeza mhitimu wa darasa la saba wa shule hiyo baada ya kupokea cheti vilivyokuwa vikitolewa na mgeni rasmi ambaye ni mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) , Dk Indiael Kaaya.

Updated: 15.09.2019 17:51
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.