Mkurugenzi IMF kung'atuka madarakani

Mkurugenzi IMF kung'atuka madarakani

17 July 2019 Wednesday 16:50
Mkurugenzi IMF kung'atuka madarakani

IFIKAPO Septemba 12, 2019 mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Christine Lagarde ataondoka madarakani 

Waziri huyo wa zamani wa Ufaransa amekuwa mkuu wa IMF tangu mwaka 2011.

Kuondoka kwake madarakani ni baada ya  kuteuliwa kuwa mkuu wa benki Kuu ya Muungano wa Ulaya (ECB).

" Kwa uwazi uliopo sasa juu ya mchakato wa kuteuliwa kama rais wa Benki kuu ya Muungano wa Ulaya (ECB) na muda utakaochukua, lazima nichukue uamuzi kwa manufaa bora ya Shirika la fedha la kimataifa ," amesema.

"Mkurugenzi mtendaji wa bodi sasa atachukua hatua muhimu zinazohitajika kuendelea na mchakato wa kumchagua mkurugenzi mpya."

Ikiwa baraza la Muungano wa Ulaya litaidhinisha uteuzi wake kuongoza ECB , atakuwa ni mwanamke wa kwanza kuwahi kuongoza benki hiyo ya Ulaya yenye jukumu la kuandaa sera ya sarafu ya Euro na masuala ya kifedha kwa ujumla katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro.

Akifahamika kama "mwamba nyota" masuala ya fedha ya kimataifa , Bi Lagarde,mwenye umri wa miaka 63, alianza taaluma ya uwakili kabla ya kuingia katika masuala ya kisiasa.

Alidumu kama waziri wa wizara kadhaa chini ya rais Nicolas Sarközy kabla ya kuchaguliwa kama Mkuu wa kwanza mwanamke wa IMF - akichukua nafasi ya Dominique Strauss Khan.

Je ni nani atayechukua nafasi ya Lagarde katika?

Uteuzi utaanza haraka. Lakini unaibua tena hoja ya mchakato wa zamani wa kumpata uongozi wa IMF na Benki ya dunia.

Alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa 5 wa IMF kutoka taifa la Ufaransa. 
Mara nyingi, Bi Lagarde ambaye amekuwa akiwekwa juu katika orodha ya wanawake 10 wenye mamlaka zaidi duniani amesaidia ku jenga upya uaminifu kwa shirika la IMF baada Ugiriki kupewa dhamana mwaka 2010, ambayo ililegeza masharti ya IMF.

Pia aliongoza utoaji wa dhamana kubwa zaidi ya IMF ya mpango wa dola bilioni 57 kwa ajili ya Argentina mwaka jana.

Mwaka jana , aliripotiwa kusema "hapana, hapana , hapana hapana, hapana hapana " alipoulizwa ikiwa anagombea uongozi wa Benki kuu ya muungano wa Ulaya (ECB).

Hata hivyo, baadae alielezea kupokea uteuzi wake kama "heshima".

Kazi yake mpya huenda ikawa kipimo cha Bi Lagarde ambaye awali alikiri kuwa hana uzoefu wa masuala ya kiuchumi. Wingu jeusi limetanda juu ya sekta ya benki ya benki ya Italia na muungano wa Ulaya unakabiliwa na hatari ya mdololo wa kiuchumi.

Hata hivyo, afisa wa zamani wa IMF amesema  uongozi wake katika masula ya fedha unamaanisha kuwa alikuwa "na uwezo wa kipekee "wa kuongoza Benki kuu ya Muungano wa Ulaya ECB.

Uzoefu wa kazi wa Christine Lagarde
1956: Alizaliwa mjini Paris
1973: Alipata ufadhili wa kusomea katika shule maalum nchini Marekani kwa mwaka mmoja, ambako alipata ujuzi wa kutosha wa lugha ya kiingereza
1981: Paada ya shule ya sheria mjini Paris, alijiunga na kampuni ya sheria ya kimataifa ya Baker & McKenzie kama mshirika, akawa mwenyekiti wake miaka 18 baadae
2005: Alikuwa waziri wa biashara wa ufaransa mwaka 2005
2007: Alikuwa waziri wa fedha wa ufaransa, akiwa mwanamke wa kwanza kuchukua wadhifa huo si Ufaransa tu bali miongoni mwa nchi zenye utajiri zaidi wa kiviwanda G8
2011: Alikuwa mkuu wa IMF
2019: Ameteuliwa kuwa rais wa benki kuu ya Muungano wa Ulaya.

Updated: 17.07.2019 17:25
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.