Ndege yagonga ndege angani 23 wajeruhiwa

Ndege yagonga ndege angani 23 wajeruhiwa

15 August 2019 Thursday 14:11
Ndege yagonga ndege angani 23 wajeruhiwa

Moscow, Urusi

NDEGE ya abiria ya Urusi imelazimika kutua kwa dharura kwenye shamba la mahindi karibu na jiji la Moscow baada ya kugonga kundi la ndege.

Watu 23 wamejeruhiwa katika tukio hilo, ambalo limesababisha ndege kutua huku injini yake ikiwa imezima na gia yake kutua ikirudi nyuma, wamesema maafisa wa afya.

Ndege hiyo Ural Airlines Airbus 321 ilikuwa ikisafiri kuelekea katika eneo la Simferopol Crimea ilipogonga kundi la ndege muda mfupi baada ya kuondoka uwanjani , hali iliyovuruga utendaji wa injini yake.

Vyombo vya habari vya taifa la Urusi vimetaja kutua kwa ndege hiyo kama "muujiza wa eneo la Ramensk".

Maafisa wa ndege hiyo wamesema ndege imeharibika sana na haiwezi kupaa tena. Uchunguzi rasmi juu ya ajali hiyo unaendelea.

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 233 na wahudumu ndani yake wakati ndege waliporipotiwa kuingia ndani ya injini na rubani wake akaamua kutua mara moja.

Abiria mmoja ambaye hakutajwa jina lake ameiambia televisheni ya taifa kuwa ndege ilianza kuyumba kwa hali isiyo ya kawaida baada ya kuondoka uwanjani.

"Sekunde tano baadaye, taa za upande wa kulia za ndege zikaanza kuwaka na kuzima na kulikuwa na harufu ya kuungua . halafu tukatua na kila mtu akatimu mbio kwenda mbali ," alisema.

Shirika la usafiri wa ndege la Rosaviatsia limesema kuwa ndege hiyo ilitua katika shamba la mahindi kilomita moja (maili 0.62 ) kutoka kwenye njia yake kwenye uwanja wa kimataifa Zhukovsky , huku injini yake ikiwa imezima na breki zake za kutua zikiwa zimerudi nyuma .

Wasafiri waliondoshwa kutoka kwenye ndege , huku baadhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu na wengine wakiongozwa kuelekea kwenye uwanja wa ndege.

Wizara ya afya imesema watoto watano walikuwa miongoni mwa wasafiri waliolazwa kufuatia ajali hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ndege ya Ural Airlines Kirill Skuratov amewaambia waandishi wa habari kuwa wasafiri waliotaka kuendelea na safari yao watawekwa kwenye ndege mbadala baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Vyombo vya habari vya Urusi vimelinganisha tukio hilo na tukio la safari ya ndege ya Marekani-US Airways iliyolazimika kutua kwa dharura katika mto Hudson muda mfupi baada ya kupaa mnamo mwaka 2009.

Migongano baina ya ndege na ndege ni jambo la kawaida katika safari za anga , huku maelfu ya ajali hizo zikitokea nchini Marekani pekee. Hata hivyo, ni nadra kusababisha ajali au kusababisha uharibifu kwenye ndege

BBC

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.