Askofu Ruwai'chi afanyiwa upasuaji

Askofu Ruwai'chi afanyiwa upasuaji

11 September 2019 Wednesday 06:57
Askofu Ruwai'chi afanyiwa upasuaji

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

RAIS John Magufuli amemjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) Jijini Dar es Salaam.

Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi alipatwa na ugonjwa wa kiharusi juzi Septemba 8, 2019 huko Moshi Mkoani Kilimanjaro ambako alianza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro (KCMC), na kisha kupelekwa MOI ambako amefanyiwa upasuaji wa kichwa na anaendelea na matibabu.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI Prof. Joseph Kahamba amesema baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali ya Baba Askofu Ruwa’ichi imeanza kuimarika.

Rais Magufuli pamoja na Madaktari na Wauguzi wa MOI wamemuombea Baba Askofu Ruwa’ichi ili apone haraka na kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akiwa katika wodi hiyo ya wagonjwa mahututi, Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa wengine waliofanyiwa upasuaji wa kichwa na kuelezea kufurahishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika taasisi ya MOI ambayo sasa inatoa matibabu ya upasuaji mkubwa ambayo hayakuwa yanapatikana nchini.

Prof. Kahamba amemshukuru Rais Magufuli kwa Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika taasisi ya MOI katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ikiwemo kukamilisha jengo, kuongeza vitanda vyote vinavyohitajika katika vyumba vya upasuaji na ICU, kununua vifaa vipya vya uchunguzi kama vile MRI, CT-Scan, Digital x-ray, Ultrasound na sasa mipango inaendelea kununua kifaa kiitwacho Endovascular Neurosuite ambacho kinagharimu shilingi Bilioni 7.5 hali iliyoiwezeshaMOI kufikia viwango vya kimataifa.

Rais Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi wa MOI kwa kazi kubwa wanayoifanya na ameahidi kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa taasisi hiyo kwa ajili ya kununulia vipandikizi kwa ajili ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu baada ya kuvunjika.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respeciuos Boniface amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa fedha hizo na kumhakikisha kuwa zitasaidia katika matibabu ya Watanzania wengi.

Akiwa njiani kurejea Ikulu, Rais Magufuli alitembelea Kituo cha Polisi cha Selander Bridge na kuzungumza na Askari wa Kituo hicho ambapo ameagiza WP 4160 Beatrice Kayuni Mlanzi kupandishwa cheo kutoka Koplo na kuwa Sajenti baada ya kuonesha utimilifu katika kazi.

Updated: 11.09.2019 07:04
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.