Bashe: Tutaweka mazingira rafiki ushiriki wa benki katika kilimo

Bashe: Tutaweka mazingira rafiki ushiriki wa benki katika kilimo

06 August 2019 Tuesday 10:02
Bashe: Tutaweka mazingira rafiki ushiriki wa benki katika kilimo

Na mwandishi wetu, Simiyu.

NAIBU Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema wakati serikali ikijiandaa kufanya marekebisho makubwa ya sera ya kilimo, taasisi za kifedha nchini zitajumuishwa katika kutoa maoni jinsi gani zinaweza kushiriki kikamilifu kwenye kilimo.

Amesema serikali kupitia wizara ya kilimo imepanga kuweka mazingira rafiki kwa taasisi za kifedha ili ziwekeze kwenye sekta hiyo, ikiwa pamoja na kuangalia mfumo gani sahihi wa utolewaji mikopo kwa wakulima.

Bashe ameyasema hayo jana wakati alipotembelea banda la Benki ya NMB kwenye maonyesho ya sikuu ya wakulima kitaifa (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Amesema lipotatizo la pembejeo hasa kwenye kilimo cha pamba na kwamba serikali kupitia bodi ya pamba inatumia fedha nyingi kuziagiza na kupelekwa kwa wakulima lakini tija haijaonekana.

“Nitakutana na taasisi zote za fedha tufanye majadiliano kwenye sera mpya ya kilimo wao wanaweza vipi kushiriki moja kwa moja mpaka kwa wakulima, wanaweza vipi kuweka mfumo mzuri na rahisi wa kutoa mikopo kwa wakulima nchini,” amesema Bashe.

“Tunahitaji benki zihusike katika kubadilisha mfumo wa kuagiza pembejeo nje, tuache kutumia mawakala na badala yake twende moja kwa moja viwandani kwa kutumia fedha zao na zitarejeshwa na wakulima mara baada ya kuvuna,” aliongeza Bashe.

Naye Mkuu wa Idara ya Biashara za serikali Vicky Bishubo kutoka NMB amesema  taasisi za kifedha kujumuishwa kwenye marekebisho ya sera hiyo ni suala muhimu.

Amesema NMB kupitia kilimo biashara (Agri-business) utakuwa wakati sahihi katika kuhakikisha wakulima na wajasiliamali nchini wanawezeshwa zaidi kupitia vikundi vyao ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji.

Aliongeza NMB inatambua kuwa inalo jukumu kubwa la kuhakikisha wakulima na wananchi wote maeneo ya vijijini, wanajumuishwa katika mfumo rasmi wa fedha kwa kupewa elimu na mafunzo.

Naye Meneja Mwandamizi katika mahusiano ya biashara ya kilimo kutoka NMB, John Mchunda  amesema benki hiyo ilitenga kiasi cha bilioni 500 kwenye kilimo- biashara kwa muda wa miaka mitano tangu mwaka 2015 kwa ajili ya kusaidia mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo na wakulima wenyewe.

"Baada ya fedha hizi kuisha mwaka jana, NMB imeongeza bilioni 500 nyingine kusaidia kukuza mnyororo wa thamani(Agricultural value Chain) kwa wakulima, Wafugaji na wavuvi na biashara zao,'' amesema.

PICHANI JUU:Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, akizungumza na wafanyakazi wa NMB kwenye banda la benki hiyo wakati wa uzinduzi wa maonesho ya nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.