Consolata alivyomuaga daktari wakati akifariki

Dk Faith alisema juzi saa kumi na moja jioni alipigiwa simu kuwa hali ya pacha hao imebadilika

Consolata alivyomuaga daktari wakati akifariki

Dk Faith alisema juzi saa kumi na moja jioni alipigiwa simu kuwa hali ya pacha hao imebadilika

04 June 2018 Monday 18:15
Consolata alivyomuaga daktari wakati akifariki

“Dk Faith sisi tunakufa,” hiyo ndio ilikuwa kauli ya mwisho ya Consolata Mwakikuti wakati pacha mwenzake, Maria akiwa katika hali ya umauti.

Dk Faith Kundy ndiye aliyekuwa akiwahudumia pacha hao katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa mpaka dakika ya mwisho walipofariki dunia juzi usiku.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi jana Jumapili, Juni 3 daktari huyo alisimulia hali ilivyokuwa katika dakika za mwisho za uhai wa pacha hao na kueleza kuwa baada ya kuona hali ya mwenzake imebadilika, Consolata alianza kumsukuma (Dk Faith) akimtaka aache kuwapatia matibabu, akieleza kuwa alikuwa katika maumivu makali na tayari alishakata tamaa.

Awali, Dk Faith alisema juzi saa kumi na moja jioni alipigiwa simu kuwa hali ya pacha hao imebadilika.

“Nilikimbia hadi wodini kwa ajili ya kuwaona na kuwahudumia. Nilipofika niliwaona wauguzi na madaktari wengine wakiendelea kutoa huduma ya kwanza hivyo niliungana nao kwa ajili ya kuokoa uhai wao,” alisema.

“Kuna dawa niliwapatia ambazo huwa zinamsaidia mtu anapokuwa anakosa hewa, Maria alikuwa ameanza kubadilika kabisa na kwa wakati huo hakuwa na ufahamu. Ilikuwa hata ukimuita haitiki wala kuonyesha kama anasikia.”

Dk Faith alisema wakati huo mfumo wa upumuaji wa Maria ulikuwa chini kabisa hivyo baada ya huduma hiyo, alirejea kwenye hali yake ya kawaida.

“Hapo Maria alifungua macho, ukimuita anaitika na akawa na hali nzuri baada ya huduma,” alisema.

Aliendelea kusimulia kuwa baada ya hali zao kuwa vizuri aliendelea kuwahudumia wagonjwa wengine hadi saa moja jioni alipoitwa tena na kuambiwa hali za pacha hao zimebadilika.

“Nilipoenda kwa mara ya pili, Maria alikuwa kwenye hali mbaya kama ile ya kwanza na safari hii hakuweza kupona. Ilikuwa kama saa mbili usiku sikumbuki vizuri dakika ila ndio muda ambao Maria alitutoka,” alisema.

Daktari huyo alisema Maria akiwa kwenye umauti, Consolata pia alianza kutetemeka na kulalamika maumivu makali mwili mzima.

“Alikuwa anaona kama hamsikii ‘ham-feel’ mwenzake na akawa ananisukuma huku akiniita kwa jina’ ‘Dk Faith sisi tunakufa’ aliniambia akisisitiza niwaache. Maria hakuweza kuongea chochote dakika za mwisho na wakati huo Consolata anasema hivyo Maria alikuwa tayari ameshafariki.”

Mwananchi

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.