Daktari Muhimbili aeleza historia ya kusikitisha ya ugonjwa uliowaua Maria na Consolata

Dk Chale alibainisha kwamba madaktari walifahamu kuwa ugonjwa huo ungekuwa na madhara kwao

Daktari Muhimbili aeleza historia ya kusikitisha ya ugonjwa uliowaua Maria na Consolata

Dk Chale alibainisha kwamba madaktari walifahamu kuwa ugonjwa huo ungekuwa na madhara kwao

05 June 2018 Tuesday 12:17
Daktari Muhimbili aeleza historia ya kusikitisha ya ugonjwa uliowaua Maria na Consolata

MKUU wa Kitengo cha magonjwa ya ndani wa hospitali ya taifa ya Muhimbili Dk Pauline Chale amesema kuwa chanzo cha vifo vya pacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti ni kusinyaa kwa mapafu hivyo kusababisha kufeli kwa upumuaji wao.

Dk Chale alibainisha kwamba madaktari walifahamu kuwa ugonjwa huo ungekuwa na madhara kwao.

“Kiutaalamu tulijua kwamba ipo siku presha ya mapafu itapanda na kusababisha shinikizo la moyo na mapafu ambapo hiyo ndiyo iliyosababisha kifo chao,” alisema  Chale ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mapafu.

Alisema walipowapokea Februari 3 katika kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), Mwaisela walikofikishwa kutokana na tatizo la kupumua lililoambatana na maambukizi ya bakteria katika mfumo wa upumuaji, jopo la madaktari lilifanya kazi mbili kubwa; kuchunguza nini kilichokuwa kinasababisha homa ya mapafu na kwa nini inashindwa kupona, “Tulianza kuchukua sampuli ya makohozi kutambua aina gani ya bakteria wanaoleta tatizo la maambukizi na kubaini ni ‘Klebsiella Pneumoniae’. Ilitusaidia kujua na kuchagua aina sahihi ya dawa, walitibiwa kwa dawa stahiki na maambukizi ya mapafu tulijiridhisha yamekwisha.”

Akifafanua alisema ili kubaini kwa nini pacha hao walikuwa na upumuaji hafifu, waliamua kufanya vipimo vya mapafu kupitia kipimo cha CT Scan ya kifua iliyoonyesha umbo la nje la kifua chao na mfumo wa njia za hewa na mapafu yenyewe ambacho kilionyesha wote wawili walizaliwa pia na ulemavu wa kifua na uti wao wa mgongo.

“Hiyo shepu ya kifua ilichangia na ushindwaji wa kupumua ambao kwao lilikuwa ni tatizo endelevu na kadri walivyokuwa wanazidi kukua, upumuaji wao ulikuwa unazidi kuwa hafifu,” alisema.

Alisema katika uchunguzi huo walibaini hata ukubwa wa mapafu ulikuwa mdogo uliobana hasa kwa Maria ambaye alikuwa chini ya mwenzake.

“Maria alikuwa na mapafu madogo sana na hata kiwango cha oksijeni kilichoingia kwenye kifua chake kilikuwa kidogo, hivyo vyote vilichangia kuendelea kusinyaa kwa mapafu yao,” alisema Dk Chale.

Alisema kutokana na hali hiyo, Muhimbili ilizungumza na familia ambayo ilitaja matatizo ambayo walizaliwa nayo tangu wakiwa wadogo. “Kwa sababu maambukizi ya mapafu yalikwishapona, tukajiridhisha wanaweza kuwachukua na kuendelea kuwatunza nyumbani, lakini inabidi wawe na vifaa maalumu vya kuweza kupumua.”

Alisema Aprili 30 waliwaruhusu lakini kutokana na maandalizi ya jinsi ya kuwafikisha Hospitali ya Mkoa wa Iringa waliondoka Mei 17 wakiongozana na muuguzi aliyebobea kuhudumia wagonjwa mahututi na daktari aliyebobea katika magonjwa ya dharura.

Dk Chale alisema kwa kipindi chote walichokuwa Iringa walikuwa wakiwasiliana na daktari bingwa, Dk Faith Kundy ambaye aliwapatia maendeleo yao.

“Daktari bingwa Dk Faith alishanipigia simu nikamwelekeza jinsi ya kufanya na aliweza kutatua kila tatizo lililotokea, lakini saa 72 kabla ya kifo chao hakukuwa na mawasiliano yoyote na kifo cha namna hiyo kinakuwa ni ghafla huwezi kujua kitakuwaje, tulijua ikifika hatua hiyo ingekuwa ni ghafla,” alisema.

Pacha hao ambao walifariki dunia Jumapili usiku mjini Iringa, watazikwa kesho kwenye makaburi ya Tosamaganga.

Azania Post

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.