Kabendera atakiwa kufika mahakamani kuelezea afya yake ilivyo

Kabendera atakiwa kufika mahakamani kuelezea afya yake ilivyo

12 September 2019 Thursday 12:14
Kabendera atakiwa kufika mahakamani kuelezea afya yake ilivyo

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu amemtaka, Erick Kabendera kufika mahakamani hapo kueleza jinsi hali ya afya yake ilivyo.

Agizo hilo limetolewa leo Septemba 12, 2019 na Hakimu, Agustine Rwizile mara baada ya kusikiliza maelezo ya pande mbili.

Mahakama ilimpa nafasi Kabendera kuelezea maumivu anayosikia ambapo akijieleza amedai hali ya kushindwa kupumua usiku bado inaendelea na siku nane zilizopita alisikia maumivu makali mguu wa kulia, maumivu makali katika mfupa ndani ya paja hali inayomfanya akose usingizi.

Amedai kuwa alionana na daktari jana na kaufanyiwa vipimo vyovyote  lakini mara ya mwisho aliomuona Alhamisi iliyopita na tiba aliyopata ni kupimwa damu na kuchomwa sindano tatu za maumivu.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu aliamuru arudi Septemba 18 ili aje kueleza kitu gani alichofanyiwa baada ya kuonana na daktari.

Awali Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Kabendera ambaye ni mwandishi wa habari umeeleza kuwa mteja wao bado anaumwa mguu anashindwa kutembea na hapumui vizuri.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amedai hayo mara baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Saimon kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Mteja wetu ni mgonjwa mpaka sasa anashindwa kutembea vizuri mguu wa kulia umepooza na anashindwa kupumua vizuri hasa usiku.”

"Mteja wetu angepata vipimo vizuri, tunaiomba Mahakama kuielekeza idara ya magereza wampe fursa ya kupatiwa matibabu hospitali yoyote ya serikali na sisi mawakili tujue anaumwa nini," amedai Wakili Kambole

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 18, 2019 na hakimu amemtaka Kabendera akaileze mahakama kuhusu afya yake. Agosti 5, 2019 Kabendera alifikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akikabiliwa na mashtaka matatu, 

Shtaka la kwanza ni kwamba kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam Kabendera na wengine ambao hawapo mahakamani anadaiwa alitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.

Inadaiwa shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa kukwepa kodi, inadaiwa kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya DAR es Salaam bila sababu za msingi alikwepa kulipa kodi Sh 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, inadaiwa katika tarehe hizo mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.

Updated: 12.09.2019 12:33
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.