Magufuli aagiza adhabu za viboko shuleni zirejeshwe

Magufuli aagiza adhabu za viboko shuleni zirejeshwe

04 October 2019 Friday 16:52
Magufuli aagiza adhabu za viboko shuleni zirejeshwe

Na mwandishi wetu, Songwe
RAIS John Magufuli ameagiza sheria kuzuia upigaji viboko wanafunzi shuleni iangaliwe upya na kwamba wachapwe viboko.

'' Nakupongeza mkuu wa mkoa wa Mbeya kwa kuwatandika viboko wanafunzi tena nimemwambia umewachapa vichache. Nafikiri kuna mahali tulikosea ile sheria ikabadilishwe wawe wanatandikwa viboko,'' amesema Magufuli leo Oktoba 4, 2019 katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Wawa mkoani Songwe.

Uamuzi huo wa Magufuli unafuatia kuwepo kwa sintofahamu iliyokuwa imetamalaki kwa  hatua aliyokuwa amechukua mkuu wa mkoa wa Mbeya,  Albert Chalamila ya kuwacharaza viboko wanafunzi 14  na kuamuru wanafunzi 392 wa kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kurudi nyumbani hadi Oktoba 18, 2019.

Aliagiza siku watakaporejea shuleni wanatakiwa kuwa na Tsh 200,000 kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa mabweni mawili ya shule hiyo yanayodaiwa kuchomwa moto na baadhi yao.

Alitoa uamuzi huo Oktoba 3, 2019 baada ya kufika katika shule hiyo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, siku moja baada ya kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa shule hiyo kwa madai ya kuchoma moto mabweni ya shule hiyo.

Chalamila alisema wanafunzi ambao hatatekeleza amri yake ya kulipa fedha kupitia benki na kutofika shuleni Oktoba 18, 2019, atafuatwa nyumbani kwa pingu na hataruhusiwa kufanya mtihani wake wa mwisho.

Na kuwa wanafunzi 14 aliowachapa viboko  ambao pia walikutwa na simu watatakiwa kulipa Tsh. 500,000 na watakaporejea shuleni waambatane na wazazi wao, kutaka fedha zote zipelekwe benki kabla ya Oktoba 18, 2019 na kupeleka risiti za malipo shuleni.

Novemba 13, 2018 serikali ilipiga marufuku mwalimu kumchapa mwanafunzi na kutembea na kiboko katika eneo la shule.

Uamuzi huo ulitangzwa  bungeni na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve (CCM).

Ole Nasha alisema utaratibu wa viboko umeainishwa vizuri katika Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002, uliotengenezwa chini ya kifungu cha 66 cha sheria ya elimu.

“Mwongozo huo pamoja na mambo mengine umeeleza dhahiri kwamba kuna makosa ambayo viboko vitatakiwa vitumike na siyo kwa kila kosa, bali kwa makosa makubwa ya kinidhamu na yenye sura ya kijinai,” alisema Ole Nasha.
 

Kuhusu viboko, alisema waraka huo unaeleza wazi kwa wakati mmoja mwanafunzi hatakiwi kuchapwa viboko vinavyozidi vinne.
“Lakini pia anayeruhusiwa kuchapa siyo mwalimu yeyote, bali ni mkuu wa shule au makamu wake au mwingine yeyote aliyepewa ruhusa hiyo kwa maandishi.

 

“Kitu kingine kinachoelezwa katika waraka huo ni kuchapa viboko lazima kibali, na kitolewe na mkuu wa shule kwa maandishi maana waraka unasema waziwazi kwamba ni marafuku mwalimu yeyote kutembea na kiboko kwa ajili ya kumchapa mwanafunzi,” alisema.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.