Magufuli aagiza matumizi mapya mradi NSSF dege

Magufuli aagiza matumizi mapya mradi NSSF dege

25 June 2019 Tuesday 12:50
Magufuli aagiza matumizi mapya mradi NSSF dege

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

RAIS John Magufuli ameagiza kutolewa kwa haraka mawazo ya  matumizi  mapya ya  majengo yaliyopo katika mradi  wa nyumba uliokuwa ukijengwa kwa ubia kati Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited katika eneo la Dege Beach Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Amesema serikali ilisimamisha mradi huo wenye nyumba zaidi ya 7,000 baada ya kubainika kuwa ni wa kifisadi na wa ovyo.

Ameeleza hayo leo Juni 25, 2019 Kigamboni jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa ghala kuu na mitambo ya gesi ya kampuni ya taifa Gas Tanzania Ltd(LPG).  Mgeni rasmi alikuwa ni rais John Magufuli.

"Mradi wa dege ulikuwa ni wa ovyo na wa kifisadi ndio maana tuliusimamisha  hivyo nataka mawazo ya haraka ya matumizi ya majengo hayo," amesema rais Magufuli

Amesema atafanya ziara rasmi katika Manispaa ya Kigamboni na kwamba agizo hilo lipatiwe majibu.

"Hatuwezi majengo kama haya yakae bure, mnaweza kushauri yakawa mabweni au nyumba za watumishi wa serikali au vinginevyo,'' amesema

Akizungumzia kuhusu matumizi ya gesi asilia nchini, rais Magufuli amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mkaa nchini.

Amesema kwa Dar es Salaam tu takribani magunia elfu 40 ya mkaa hutumika kwa siku na kwamba inachangia kuharibu mazingira hasa miti.

Kampuni ya LPG iliyowekeza nchini kwa kuzalisha na kuuza gesi maalumu kwa matumizi ya nyumbani  inatarajia kutumia takribani bilioni 500 katika kipindi cha miaka mitatu. Inauza gesi hiyo ndani na nje ya nchi.

Mkataba kati ya NSSF na Azimio Housing Estate Limited (AHEL) ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni hodhi ya “Hifadhi Builders” ambapo AHEL ilikuwa na asilimia 55 na NSSF asilimia 45. Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa kwenye mradi na asilimia 35 angetakiwa kuweka fedha taslimu.

Mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba 7,460 ambapo jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani 653,436,675 ambazo kati yake ujenzi ungegharimu Dola 544,530,562 wakati gharama za ardhi zingekuwa Dola 108,906,113. Kwa fedha za Tanzania mradi pamoja na ardhi ungegharimu  trilioni 1.5.

Hadi kufikia Juni 2018 NSSF  walikuwa wameshailipa  kampuni ya Hifadhi Builders Dola 133,838,662.2 kama mchango wake kwenye ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na bilioni 305.8 wakati kampuni ya Azimio ikitoa Dola 5,500,000 sawa na bilioni 12.6 tu.

Updated: 25.06.2019 13:50
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.