banner68

Magufuli: Walipe ndani ya mwezi mmoja au wakamatwe haraka

Kiasi cha shilingi bilioni 38 bado kinadaiwa, na kinapaswa kurudishwa ndani ya mwezi mmoja

Magufuli: Walipe ndani ya mwezi mmoja au wakamatwe haraka

Kiasi cha shilingi bilioni 38 bado kinadaiwa, na kinapaswa kurudishwa ndani ya mwezi mmoja

17 May 2018 Thursday 14:18
Magufuli: Walipe ndani ya mwezi mmoja au wakamatwe haraka

Na Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli ametoa mwezi mmoja kuanzia leo kwa taasisi zote zinazoidawa mikopo ya matrekta yaliyokuwa yanatolewa na Jeshi la Wananchi kupitia SUMA JKT kulipa mara moja au kuwa tayari ‘kucheza muziki.’

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha uwekezaji cha Suma JKT kilichopo eneo la Mgulani jijini Dar es Salaam mchana huu alisema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 38 bado hazijarudishwa.

Alisema kuwa waliochukua mkopo huo, hata kama ni watu binafsi, taasisi ya umma, jeshi lenyewe au ikulu hawana budi kulipa ndani ya mwezi mmoja.

Alimuagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kuwaandikia wadaiwa wote sugu na kumpatia nakala ya barua yeye ili aendelee kufuatilia.

Alisema kuwa kuna usemi unasema kukopa harusi na kulipa matanga, lakini yeye anataka iwe kukopa harusi kulipa harusi.

Aliongeza kuwa fedha hizo zikipatikana zitasaidia sana kwa ajili ya kuanzisha viwanda vingine ili kuwafanya wanajeshi wasiendelee kuomba.

Aliviagiza vikosi vyote vya ulinzi na usalama likiwemo jeshi lenyewe kwa kutumia askari wake kuwasaka wote watakaoshindwa kurejesha mkopo huo ndani ya mwezi mmoja.

Alitaka kukoma kwa tabia ya kulichezea jeshi kwani ni dharau kubwa na hilo kamwe haliwezekani.

Aidha alibainisha kuwa idara ya ulinzi ya JKT, yaani Sum Guard nayo inadai taasisi mbali mbali zaidi ya shilingi bilioni 3.4 na kuagiza pia nazo zilipwe ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Amiri jeshi alisema kuwa serikali itaendelea kuwakumbuka wanajeshi na kuwaomba kufanya kazi kwa moyo wa kizalendo.

Pia aliamuagiza Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Venance Mabeyo kumpatia orodha ya wakuu wa jeshi wastafu ili aweze kuwateua kuongoza bodi mbali mbali.

Alisema kuwa ana bodi nyingi sana na akaomba wamletee majina hayo haraka na kuongeza kuwa anaamini hawatakataa.

Kuhusu kiwanda hicho alisema kuwa amefurahishwa sana na uwekezaji huo ambao kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuongeza kipato.

Aliseme kuwa kuanzia leo atakuwa mdau wa maji ya chupa aina ya Uhuru Peak yanayotengenezwa na kiwanda hicho.

Alisema kuwa atashangaa sana endapo akienda Wizara ya ulinzi, kwa mkuu wa majeshi, polisi, magereza uhamiaji, takukuru na mkuu wa mkoa asipokuta maji ya Uhuru.

Aliongeza kuwa angekuwa na amri basi angeagiza taaasisi zote nchini kutumia maji hayo, lakini asipoyakuta kwenye zile alizozitaja atashangaa tu.

Kuhusu changamoto za jeshi, alisema kuwa serikali itaendelea kuzitatua kadiri uwezo utakavyoruhusu.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.