banner58

Mbowe: Bunge liache siasa kwenye mazishi ya Bilago, familia iachwe

Ni kutokana na kuwepo kwa mvutano baina ya Chadema na Uongozi wa Bunge wakati wa shughuli za mazishi ya Mbunge Kasuku Bilago

Mbowe: Bunge liache siasa kwenye mazishi ya Bilago, familia iachwe

Ni kutokana na kuwepo kwa mvutano baina ya Chadema na Uongozi wa Bunge wakati wa shughuli za mazishi ya Mbunge Kasuku Bilago

29 May 2018 Tuesday 16:09
Mbowe: Bunge liache siasa kwenye mazishi ya Bilago, familia iachwe

Na Mwandishi Wetu

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amelitaka Bunge kuacha siasa kwenye suala la mazishi ya Mbunge wa Buyungu mkoani Kigoma anayejulikana kama Kasuku Bilago (Chadema) na kuichia familia iendeshe msiba kwa jinsi inavyotaka.

Akizungumza mchana huu kwenye viwanja vya bunge jijini Dodoma wakati wa kuuga mwili wa marehemu Bilago, Mbowe alisema kuwa familia na wananchi wana haki ya kumzika.

Alisema kuwa familia na wapiga kura wake wana haki ya kumzika mpendwa wao, na kutaka kuacha kupolitizice (husisha siasa) mazishi hayo.

Alisema wao Chadema walipenda kumzika marehemu Bilago siku ya Jumamosi, lakini familia imekaa na kuamua kumzika Alhamisi, badala ya kesho kama inavyotajwa na bunge.

Kiongozi huyo alisema kuwa ni jambo la ajabu kuona kuwa Chadema wametoa ratiba ya mazishi na bunge kuja na ratiba yake.

Alisema kuwa bunge haliwezi kupoka mamlaka na iachwe familia jinsi ilivyoamua mpendwa wao azikwe.

Aliongeza kuwa msiba huo ni mzito sana na kuwa kifo kitumike kuleta upatanisho na kutafakari maisha ya binadamu kila siku.

Alisema kuwa utukufu na vyeo vyote vina mwisho na kuwa hakuna sababu ya kuumizana sisi kwa sisi.

Aidha Mbowe, alisema kuwa wamepeana mikono kutakiana heri kwenye ibada ya kumuombea marehemu, kitendo hicho kisiwe cha unafiki.

Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alisema kuwa bunge halina sababu ya kupoka madaraka ya familia kuhusu mazishi hayo.

Alisema kuwa awali kamati ya bunge ya uongozi ilikaa na tume ya bunge na wakaafikiana kuwa mazishi yafanyike kesho Jumatano.

Hata hivyo alibainisha kuwa taarifa za kuwa mazishi yatafanyika Alhamisi zilifika baada ya kukaa kwa kikao hicho.

Lakini alidokeza kuwa halijaharibika jambo kwani kila kitu kitakwenda jinsi chama, uongozi wa familia na bunge lilivyojipanga.

Alimtaka kiongozi wa kambi ya upinzani wa Bungeni kuondoka kwa amani kwani akienda Kigoma atakutana na Spika na hakutaharibika neno.

Awali alisema kuwa taarifa za msiba wa mbunge huyo wamezipokea kwa mstuko mkubwa kwani wenzake wengi walikuwa hawajui kama anaumwa.

Alisema kuwa huyo ni mbunge wa nne kufariki katika bunge hili, na msiba huu umewapiga sana wabunge wote.

Kasuku Samson Bilago,  alizaliwa miaka 54 iliyopita ameacha mke na watoto watatu, amewahi kufanya kazi ya ualimu kwa zaidi ya miaka sita, na alikuwa katibu wa umoja wa vijana wa CCM kabla ya kujiunga na Chadema.

Azania Post

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.
Avatar
Iman 2018-05-30 20:39:30

R.ip.