Museveni: Tanzania ndio Hijja yangu ya kisiasa

Museveni: Tanzania ndio Hijja yangu ya kisiasa

13 July 2019 Saturday 15:43
Museveni: Tanzania ndio Hijja yangu ya kisiasa


Na mwandishi wetu, Chato
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amesema Tanzania ndio sehemu ya kufanyia Hijja yake ya  kisiasa.

Amesema hayo leo Julai 13, 2019 wilayani Chato mkoani Geita mara baada ya kuwasili kwa ndege akitokea nchini Botswana. Yupo nchini kwa ziara ya siku moja ya kibinafsi

"Kila mwaka Waislam wanakwenda Hijja nchini Saudia Arabia kutekeleza ibada yao, Wakristo nao wana Hijja zao wengine wanakwenda Vatican Italia na mimi Hijja yangu ya kisiasa ni Tanzania,'' amesema Museveni

Amesema tangu uongozi wa rais wa kwanza hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi sasa Tanzania imeendelea kuwa kimbilio la wanasiasa wengi barani Afrika.

Museveni amesema pamoja na mambo mengine uwanja wa ndege wa Chato utarahisisha shughuli za kibiashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda.

''Hata wananchi wa Uganda huwa napenda kuwaelimisha kuwa tukizungumza maendeleo namaanisha ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na vingine vingi vinavyotumiwa na watu wote na ukizungumzia utajili au mali hizo ni juhudi za mtu binafsi,'' amesema

Naye Rais John Magufuli amesema Tanzania na Uganda zinahistoria ambayo haitosahaulika  na kumtaka Museveni aongee na wafanya biashara wa nchini mwake kuutumia uwanja wa ndege wa Chato kwa safari na biashara.

"Uwanja huu upo karibu na Uganda yaani Entebe na ni njia fupi ya kuingia(kufika) Uganda ni muhimu ikatumika ipasavyo kwa wasafiri na wafanyabiashara,'' amesema Magufuli

Rais Magufuli amempongeza Museveni kwa uamuzi wake mgumu wa kuridhia bomba la mafuta kutoa Ohima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

"Nakupongeza kwa uamuzi wako mgumu wa kuruhusu bomba la mafuta kupita Tanzania, hii itasaidia kuchochea maendeleo na hata pia kwa wananchi wote wanatakaopitiwa na bomba hilo,'' amesema

Baada ya hafla hiyo fupi wawili hao walielekea nyumbani kwa rais Magufuli katika kijiji cha Mlimani wilayani Chato.

Wakiwa hapo, wawili hao watafanya mazungumzo. Rais Magufuli yupo kijijni kwao kwa mapumziko.  

Updated: 13.07.2019 15:56
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.