Rais Magufuli ataja sababu za kumfuta kazi January Makamba

Rais Magufuli ataja sababu za kumfuta kazi January Makamba

22 July 2019 Monday 10:22
Rais Magufuli ataja sababu za kumfuta kazi January Makamba

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
RAIS John Magufuli ametaja miongoni mwa sababu zilizopelekea kumfuta kazi January Makamba na kumteua George Simbachawene kushika nafasi ya waziri wa nchi, ofisi ya makamu wa rais(Muungano na Mazingira)

Vile vile,  ameelezea sababu ya kumteua Hussein Bashe katika nafasi ya Naibu Waziri wa Kilimo.

Akizungumza leo Julai 22, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwaapisha viongozi hao, rais Magufuli amesema taarifa zisizo za kweli, uzembe na ucheleweshaji wa utekelezaji majukumu katika wizara ya Mazingira ndio sababu ya kufikia uamuzi huo.

 "Katika wizara ya Mazingira kulikuwa na miradi hewa, ucheleweshaji wa kutoa vibali kwa wewekezaji hasa kutoka Nemc na ucheleweshaji wa makusudi wa utekelezaji maagizo,'' amesema rais Magufuli na kuongeza

"Utekelezaji wa agizo la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki umechukua miaka minne, nilitoa agizo, makamu wa rais akatoa, waziri mkuu akatoa lakini wapi ndipo nilipotoa amri ya lazima, ndio mwishoni ikatekelezwa. Waziri Simbachawene usiwe kama hivyo, simamia na urahisishe mambo''

Pamoja na mambo mengine amemtaka waziri Simbachawene akawe chachu ya kuimarisha muungano na si kuuzorotesha.

Kuhusu uteuzi wa Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega mkoani Tabora, Rais Magufuli amesema "Bashe ulipokuwa Bungeni nilikuwa nasikiliza kwa makini uchambuzi wako (Analysis) katika masuala ya kilimo, nikavutiwa sana ndio maana nimekuteua ili ukawasilishe kivitendo yote uliyokuwa ukiyachambua.''

Rais Magufuli amesema sekta ya kilimo inachangamoto nyingi ikiwemo wizi na kwamba bodi ya sukari inapigwa vita. "Nilikuwa nasubiri waziri aivunje bodi ya sukari ili nimshughulike lakini hajafanya hivyo.Bodi hii inafanya mambo makubwa na inakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara'' aliongeza rais

Amemtaka Bashe ahakikishe wananchi wananufaika  na mazao ya kilimo. "Sekta ya kilimo inachangamoto lakini nataka kilimo kilete tija, Mkoani Kagera kuna tatizo la uuzaji wa kahawa kuna wafanyabiashara wachache wanaanza kuwadanganya wakulima, nataka washughulikiwe kwa mkono mrefu wa serikali,'' ameagiza rais Magufuli.

Awali mara baada ya kuapishwa Simbachawene amesema  "Rais Magufuli nashukuru kwa dhati kuniamini tena na kunipa nafasi hii tena, nafahamu nchi inamatatizo  mengi katika mazingira.  Fedha haziendi kutatua moja kwa moja matatizo ya mazingira  zaidi zinakwenda katika eneo la utawala japo fedha zinazotajwa kuingi katika nchi ni nyingi lakini hazitatua kero na changamoto za mazingira na kuyaokoa.

''Mazingira ndio uhai wetu shughuli zote za kiuchumi na kimaisha zinahitaji mazingira japo vyanzo vingi ikiwemo vya maji vinatoweka,'' 

Kuhusu masuala ya Muungano, Simbachawene amesema "Nahitaji kujifunza japo mimi ni mwanasheria lakini najua msingi wa muungano wetu ni wa kihistoria kuliko maandishi, natumai nikiingia ofisini nitajifunza na kufundishwa.

Naelewa maana ya wewe kuniteuwa nashukuru kwa kuniteua najua maana ya kula kiapo hiki ni kiapo changu cha tano'' 

Kwa upande wa Bashe amesema" Nashukuru kwa imani ulionyesha kwangu na imani hii ni utumishi kwa wananchi. najua changamoto zilizopo katika kilimo nimejifunza kupitia kamati ya Bunge na maandishi
Najua asilimia 40 hadi 60 ya wanyonge wa nchi hii wapo katika sekta ya kilimo na najua kilimo ni biashara na uchumi''

Simbachawene ambaye pia ni Mbunge  wa Kibakwe  mkoani Dodoma na mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Bajeti. Septemba 7, 2017 alitagaza kujiuzulu uwaziri wa Tamisemi baada ya rais  Magufuli kuwataka wote waliotajwa kwenye ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi iliyoundwa na Bunge  kuonyesha walivyolisababishia hasara taifa.

Simbachawene ameitumikia serikali ya awamu ya nne na tano kwa vipindi tofauti. Mwaka 2012 Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na mwaka 2014 alimuhamishia wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Januari 2015 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini baada ya aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Prof. Sospeter Muhongo kujiuzulu kutokana na kashfa ya Escrow.
Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani alimteuwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Tamisemi) kabla ya kujiuzulu kwake Septemba 7, 2017.

Updated: 22.07.2019 10:41
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.