Sakata la Azory Gwanda,Waziri Kabudi aibua sintofahamu!

Sakata la Azory Gwanda,Waziri Kabudi aibua sintofahamu!

11 July 2019 Thursday 09:24
Sakata la Azory Gwanda,Waziri Kabudi aibua sintofahamu!

WAZIRI wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mwandishi, Azory Gwanda  'alitoweka na kufariki'.

Katika mahojiano na BBC katika kipindi cha FOCUS ON AFRICA mjini London waziri Kabudi pia amesema visa vya watu kutoweka vimesababisha uchungu mwingi nchini humo.

''Wacha nikwambie unapozungumzia kuhusu kisa hicho, ni mojawapo ya visa ambavyo vimesababisha uchungu mwingi nchini Tanzania''.
Aliendelea: Katika eneo la Rufiji sio tu Azory Gwanda aliyetoweka na kufariki, nataka kukuhakikishia kwamba tunachukua kila hatua sio tu katika eneo la Rufiji bali pia maeneo mengine ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa watu wetu wako salama-sio tu waandishi bali pia Polisi na raia wa kawaida.

Baada ya mahojiano hayo wanaharakati wa haki za binadamu na raia wamesambaza kanda ya video ya mahojiano hayo mitandaoni wakimtaka waziri huyo kuelezea familia ya mwandishi huyo ni wapi mwili wake ulipatikana.

Wakili maarufu nchini humo Fatma Karume maarufu Shangazi aliandika katika mtandao wake wa twitter: Mungu wangu Palamagamba amekiri katika BBC FOCUS ON AFRICA kwamba Azory alitoweka na kufariki. Je alijuaje kwamba amefariki?

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa awali na kampuni ya magazeti ya mwananchi, mwanahabari huyo wa kujitegemea alitoweka Novemba 21, 2017.

Gwanda alikuwa anaishi na kuripoti kutoka mji wa Kibiti wilayani Rufiji mkoani Pwani, ambao upo kilomita takriban 130 kusini mwa jiji la  Dar es Salaam.

Gwanda ni mmoja wa waaandishi wa kwanza kabisa kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa mji huo na kuzua hofu kubwa.

Mke wake Anna Pinoni alisema watu wapatao wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walimchukua Gwanda kutoka katikati ya mji huo, mahali ambapo hupendelea kukaa.

Anasema pia aliporudi nyumbani alikuta vitu vimezagaa, ishara kwamba inawezekana waliipekua nyumba yao.

Azory aliwasiliana na ofisi za Mwananchi mara ya mwisho  Novemba 20 kwa majukumu ya kikazi.

Mjadala kuhusu kutoweka kwa mwandishi huyo wa uchunguzi ulitanda kila sehemu nchini humo huku waziri wa habari wa Tanzania akiliambia bunge kwamba kesi yake ni hafifu kwa kuwa alipotea eneo ambalo mamia ya Watanzania walipotea.

"Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea, hawauliziwi hao ila mmoja huyo ndiyo dhahabu."

"Halafu inaulizwa Serikali ambayo imeshughulikia kwa kiasi kikubwa na maofisa wa Serikali wengi wamekufa pale, najua mnawalisha Wazungu na wafadhili matangopori, hatujakosa chochote acha tushushwe madaraja, sisi tunaheshimu uhuru wetu kwanza," alinukuliwa akisema.

Tayari muungano unaopigania umoja wa vyombo huru vya habari unaoshirikisha makundi 30 kote duniani umeutaka uatawala kuwajibika.

Serikali imedai kuchunguza kesi yake na za watu wengine waliotoweka lakini hakuna kilichoafikiwa hadi sasa.

PICHA JUU: Waziri Palamagamba kabudi

PICHA CHINI; Azory Gwanda

BBC

Updated: 11.07.2019 15:41
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.