Serikali yaanzisha mradi mpya wa kuunganishiwa umeme

Serikali yaanzisha mradi mpya wa kuunganishiwa umeme

05 August 2019 Monday 09:30
Serikali yaanzisha mradi mpya wa kuunganishiwa umeme

Na Veronica Simba, Pwani 
SERIKALI imeanzisha rasmi mradi mpya wa umeme unaolenga kupeleka nishati katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa miji.

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani kwa nyakati tofauti, amezindua mradi husika unaojulikana kwa jina la kigeni kama ‘Peri-Urban’ katika Wilaya tofauti za Mkoa wa Pwani na kuwa gharama ya wananchi kuunganishwa ni sawa na ile ya umeme vijijini yaani shilingi 27,000 tu.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Agosti 4, 2019, Dk Kalemani alisema Serikali iliamua kuandaa mkakati maalum wa kupeleka umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji ambayo yalibainika kurukwa na miradi mbalimbali ya umeme.

“Mradi huu ni mahsusi kwa ajili ya maeneo ambayo yako mijini lakini yana sura ya vijiji; yaani yako pembezoni mwa miji.”

Alisema serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza mradi huo na kuwataka wananchi katika maeneo yote ambako utatekelezwa, wachangamkie fursa hiyo kwa kujitokeza kulipia ili waunganishiwe umeme.

Gharama za kutekeleza mradi huo wilayani Mkuranga ni bilioni 11.5, Wilaya ya Kisarawe  bilioni 25 na Wilaya ya Kigamboni bilioni 9.32 ambazo zote ni fedha za ndani. 

Hizo ni Wilaya ambako tayari mradi umezinduliwa rasmi lakini zoezi hilo linaendelea katika maeneo mengine mbalimbali nchini.

Miongoni mwa maagizo hayo ni kuhakikisha mradi unatekelezwa ndani ya kipindi kilichoainishwa katika mkataba ambacho ni miezi tisa na kwamba muda hautoongezwa.

Vilevile, Waziri aliwataka wakandarasi husika, kuajiri wananchi wa maeneo husika ambako mradi unatekelezwa na kuwalipa ujira wao kwa wakati. Akifafanua, alisema ajira hizo ni zile zisizohitaji taaluma maalum kama vile kuchimba mashimo, kufukia nguzo na nyingine za aina hiyo.

Pia, aliagiza wananchi wenye nyumba zisizozidi vyumba vinne, wagawiwe vifaa vya Umeme Tayari (UMETA), ili kuwapunguzia gharama za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme.

Alisema vifaa hivyo vimetolewa bure na serikali kwa idadi ya 250 kila eneo na kwamba vikiisha, wananchi watauziwa kwa gharama ndogo ya shilingi 36,000 tu.

Waziri alizindua mradi wa ‘Peri-Urban’ Agosti 4 (Mkuranga), Agosti 3 (Kisarawe) na Agosti 2 (Kigamboni) mwaka huu (2019). Mradi huo utazinduliwa wilayani Kibaha na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Agosti 5 ambapo zoezi litaendelea katika maeneo mengine mbalimbali.

PICHANI JUU:Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza huku akiwa ameshika kibatari alichokabidhiwa na wananchi wa Mkuranga, mkoani Pwani wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa umeme ujulikanao kama ‘Peri-Urban’ Agosti 4, 2019. Kibatari hicho ni ishara ya wananchi wa Mkuranga kuachana na matumizi yake na kutumia umeme utakaounganishwa ndani ya kipindi cha miezi tisa.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.