Tundu Lissu : Jaji Sirillius ‘amechemsha’

Tundu Lissu : Jaji Sirillius ‘amechemsha’

09 September 2019 Monday 19:26
Tundu Lissu : Jaji Sirillius ‘amechemsha’

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

ALIYEKUWA mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema Jaji aliyetoa hukumu kwa kukataa maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma, amekosea kisheria.

Leo Septemba 9, 2019 Jaji wa Mahakama Kuu, Sirillius Matupa alitoa hukumu hiyo akisema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Na kwamba kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Akizungumza na Azaniapost kwa njia ya simu, Lissu amesema hakuwa na ugomvi na tume ya taifa ya uchaguzi(Nec) wala mgombea yoyote hivyo asingeweza kufungua kesi kupinga uchaguzi.

‘‘Jaji aliyetoa hukumu amekosea kisheria, mimi(Lissu) sina ugomvi na Nec, wala mgombea yeyote aliyejitokeza. Ugomvi wangu wa kisheria ni dhidi ya uamuzi wa Spika Ndugai kama ulikuwa ni sahihi au la,’’ amesema Lissu na kuongeza

‘‘Hivyo jibu lolote katika hayo lingetoa taswira na kubadilisha kila kitu na kwamba hoja kutakuwa na wabunge wawili si kweli’’

Kuhusu hatma ya hukumu hiyo, Lissu amesema sio mwisho wa mapambano yake ya kupigani haki yake na kwamba atakwenda Mahakama ya Rufani.

‘‘Pamoja na hukumu hii lakini sitorudi nyuma, nitaendelea kupigania haki yangu na nitakwenda Mahakama ya Rufani,’’ amesema

Katika maombi yake ya namba 18 ya mwaka 2019 dhidi ya Spika wa Bunge, Mwanasheria Mkuu(AG) Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake na mahakama itengue taarifa hiyo

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya katiba ya nchi.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.