Wahujumu uchumi 467 kuachiwa huru, bilioni 107.842 zapatikana

Wahujumu uchumi 467 kuachiwa huru, bilioni 107.842 zapatikana

30 September 2019 Monday 10:37
Wahujumu uchumi 467 kuachiwa huru, bilioni 107.842 zapatikana

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

JUMLA ya watuhumiwa 467 wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wameandika barua ya kuomba msamaha wa kusamehewa makosa hayo na wamekubali kulipa takribani Tsh bilioni 107.842.

Vilevile watuhumiwa wengine wa kesi hizo wameongezewa siku saba zaidi kuanzia leo Septemba 30, 2019 na kwamba ofa hiyo ni kwa ajili ya walioandika barua na bado hazijafika katika ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).

‘‘Huu ni msamaha wa kweli. Ninaongeza siku saba na sitoongeza wala kutoa msamaha huu tena. Wakilipa fedha zao ni vizuri waachiliwe na wakakae na familia zao lakini utokaji wao ufuate taratibu za kimahakama kwa kuwa walikamatwa kisheria,’’ amesema rais John Magufuli leo Septemba 30, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokea taarifa ya msamaha kutoka kwa DPP

Rais Magufuli amewataka wote wenye nia ya kukiri na kutubu makosa ya uhujumu uchumi wasihofu na wasidanganywe, watumie fursa hiyo na kwamba watasamehewa.

‘‘Sio kwamba kesi za uhujumu uchumi zimefutwa zipo kisheria na ninaonya yoyote atakayekamatwa kuanzia leo kwa tuhumu za uhujumu uchumi hato samehewa,’’ amesema Magufuli

Awali akikabidhi taarifa ya utekelezaji wa ushauri uliotolewa na rais Magufuli Septemba 22, 2019, DPP Biswalo Mganga amesema jumla ya watuhumia 467 wa kesi za uhujumi uchumi wamekiri makosa hayo na kukubali kulipa takribani bilioni 107.842.

Katika fedha hizo baadhi ya watuhumiwa wamekubali kulipa bilioni 94 kwa awamu huku watuhumiwa wengine wamekubali kulipa bilioni 13 moja kwa moja.

‘‘Katika fedha hizo jumla ya bilioni 78.9 na zingine Dola za kimarekani elfu 25.6(Sawa na bilioni 5.17) zipo tayari kulipwa muda wowote,’’ amesema DPP huyo

DPP Mganga amesema Septemba 28, 2019 mmoja wa watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam alikiri makosa yake hayo na kulipa moja kwa moja dola za kimarekani laki 4.5 sawa na bilioni1.36

‘‘Hata hivyo pamoja na kulipa fedha hizo papo hapo pia alilipa faini ya milioni 3,’’ amesema

Aidha, DPP Mganga amesema katika siku za hivi karibuni dhahabu yenye gram 33.2 ilikamatwa na jumla ya vito yenye gram 35 ikiwemo gram 18 za Tanzanite.

Kuhusu Magufuli kuongeza siku saba, hatua yake ilifuatia baada ya ombi la DPP Mganga kutaka ziongezwe siku tatu kuanzia leo Septemba 30, 2019 kwa watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi ili barua zao zimfikie.

Mganga amesema zoezi hilo ni la kisheria na watalifanya kwa mujibu wa taratibu za kisheria ili serikali isipate madhara yoyote

Updated: 01.10.2019 10:57
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.