Waziri aagiza mkadarasi akatwe mshahara

"Mkurugenzi TANESCO fuatilia, ukikuta kuna uzembe, wakate asilimia 10 ya mshahara wao maana wanataka kutucheleweshea mradi".

Waziri aagiza mkadarasi akatwe mshahara

"Mkurugenzi TANESCO fuatilia, ukikuta kuna uzembe, wakate asilimia 10 ya mshahara wao maana wanataka kutucheleweshea mradi".

19 May 2019 Sunday 08:01
Waziri aagiza mkadarasi akatwe mshahara


Na Veronica Simba - Tanga
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata asilimia 10 ya malipo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga, endapo itabainika hana sababu za msingi kuchelewesha mradi.


Ametoa maagizo hayo Mei 18, 2019 katika Kijiji cha Vuo, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.


Akizungumza na wananchi wa Vuo, kabla ya kuwawashia rasmi umeme, Dkt. Kalemani alisema kasi ya mkandarasi hairidhishi maana ni ndogo sana hivyo akawataka watendaji wa TANESCO kufuatilia ili kujiridhisha endapo kuna sababu za msingi za ucheleweshaji huo wa mradi.


"Mkurugenzi TANESCO fuatilia, ukikuta kuna uzembe, wakate asilimia 10 ya mshahara wao maana wanataka kutucheleweshea mradi." amesema


Sambamba na agizo hilo, Waziri alielekeza mkandarasi huyo kuwa na Mpango-Kazi wenye mchanganuo wa kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki.


Kufuatia agizo hilo, alimtaka Meneja wa TANESCO wa Wilaya, kumwandikia barua ya kusitisha mkataba wake, Mkandarasi husika endapo atashindwa kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki.


Aidha, Waziri alimtaka Meneja huyo pamoja na Mkandarasi kuwasilisha maelezo ndani ya siku moja sababu za kusuasua kwa utekelezaji wa mradi.


“Meneja wewe ndiye wa kumsimamia Mkandarasi. Kama kasi yake ni duni, inamaanisha hata wewe utendaji wako siyo mzuri,” alisema Waziri.


Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alibainisha kuwa moja ya sababu za Mkandarasi kuwa na kasi ndogo yawezekana kuwa ni uhaba wa vibarua alioanao.


Alimtaka kuongeza idadi ya vibarua mara moja na kwamba vibarua hao watoke eneo husika na awalipe ujira wao kwa wakati.


“Ni marufuku kuajiri vibarua nje ya eneo unakotekelezwa mradi. Vibarua wote wawe wa eneo husika ili wanufaike kwa uwepo wa mradi katika eneo lao.”


Akizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkinga, Pangani na Muheza, ambako alikagua utekelezaji wa miradi ya umeme pamoja na kuwasha umeme katika vijiji kadhaa; Waziri Kalemani alitoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ambazo ni shilingi 27,000 tu.


Aidha, aliwataka wale ambao tayari wameunganishiwa umeme, kuutumia kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ili wanufaike kwa kuinua kipato na kuboresha maisha yao.


Waziri alitoa zawadi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA), kwa wananchi katika maeneo yote aliyotembelea ili kuwahamasisha kuchangamkia fursa ya uwepo wa mradi wa umeme vijijini na hivyo kujitokeza kwa wingi kulipia na kuunganishiwa nishati hiyo.


Katika Shule ya Sekondari Bushiri wilayani Pangani, Waziri alikabidhi vifaa 40 vya UMETA kwa wanafunzi na walimu, ili vifungwe katika vyumba vya madarasa, maabara, ofisi, nyumba za waalimu, vyoo na barabara zote za shule ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha usalama wa watoto, hususan wa kike.


Waziri anaendelea na ziara yake mkoani Tanga ambapo anatarajiwa kuhitimisha kwa kutembelea Wilaya ya Korogwe.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.