Waziri amvua cheo meneja wa Tanesco

Waziri amvua cheo meneja wa Tanesco

15 September 2019 Sunday 06:34
Waziri amvua cheo meneja wa Tanesco

Na Veronica Simba - Geita

WAZIRI wa Nishati Dk Medard Kalemani amemvua madaraka, meneja wa Tanesco wilayani Bukombe mkoani Geita, Thadei Mapunda kutokana na utendaji kazi usioridhisha. Ametoa agizo hilo Septemba 14, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo.

“Mkurugenzi Mtendaji Makao Makuu, sijaridhishwa na utendaji kazi wa Meneja wa Wilaya hii. Naagiza muweke pembeni sasa hivi. Huyu siyo Meneja wa hapa kuanzia leo,” aliagiza Waziri.

Akizungumza na wananchi wa Bukombe, katika uwanja wa stendi ya zamani, Waziri Kalemani alisema uamuzi wake huo unatokana na sababu kadhaa ikiwamo malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wilayani humo kutokupatiwa huduma ya umeme pasipo sababu za msingi.

“Nimepita Kapela, kuna nyumba nzuri, kubwa lakini hazina umeme. Ni masikitiko makubwa sana, Halafu namuuliza Meneja hizi nguzo zimechimbiwa lini; ananiambia mwezi uliopita wakati nauona ni udongo wa leo na jana.”

Katika hatua nyingine, Waziri alisisitiza kuwa gharama za kuunganishiwa umeme vijijini ni shilingi 27,000 na kuwaonya mameneja wa TANESCO nchi nzima kutowalipisha nguzo wananchi vijijini.

Aidha, kabla ya kwenda kuzungumza na wananchi hao, Waziri alipita maeneo mbalimbali kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, ambayo ni pamoja na soko kuu na kuagiza iwekwe transfoma na maduka yaliyopo eneo hilo yaunganishiwe umeme ndani ya siku moja.

Vilevile, Waziri alitoa siku 30 kwa mameneja wa TANESCO wa Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa, kwa kushirikiana na mkandarasi, kuhakikisha maeneo ya Nifa, Majengo, Kerezia, Maghorofani, Stendi Kuu na Stendi ya Mabasi yawe yamewashiwa umeme ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, alimshukuru na kumpongeza Waziri Kalemani kwa kazi kubwa anayoifanya.

“Ninao ujasiri na imani kwamba, chini ya Dk Kalemani, wananchi wa Bukombe, maswali yenu ya umeme yamepata majibu leo,” alisema.

PICHANI: Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria uwashaji wa umeme Kijiji cha Igulwa, wilayani Bukombe, Septemba 14, 2019. Kulia kwake ni Mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini Doto Biteko na kushoto kwake ni bibi mwenye nyumba iliyowashiwa umeme, Elizabeth Herman.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.