Waziri January, Kigwangala 'watifuana' kupitia mtandao wa kijamii

Waziri January, Kigwangala 'watifuana' kupitia mtandao wa kijamii

08 July 2019 Monday 21:43
Waziri January, Kigwangala 'watifuana' kupitia mtandao wa kijamii

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mpango wa kuanzisha magari ya kutumia nyaya kukwea Mlima Kilimanjaro umechukua sura mpya baada ya mawaziri wawili husika nchini kupishana kauli mitandanoni.

Mpango huo ulitangazwa mwezi Aprili na Waziri wa Utalii na Maliasili Hamisi Kigwangala ili kukuza maradufu idadi ya watalii wanaoukwea mlima huo na kuongeza pato la taifa hilo ambalo linategemea kwa kiasi kikubwa sekta hiyo.

Hata hivyo, kumekuwa na mashaka juu ya hali ya kimazingira katika mlima huo endapo magari hayo yatakubaliwa kufanya kazi.

Mwishoni mwa juma, Waziri wa Mazingira , January Makamba aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa ofisi yake ndiyo itakayotathmini hali ya kimazingira kabla ya kutoa kibali kwa ujenzi wa mradi huo.

Kigwangala alijibu kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kudai kuwa 'watu wa Mazingira wanataka kuingilia mradi' huo.

Ujumbe huo ulifungua ukurasa wa 'vita ya maneno' baina ya mawaziri hao na kuchagizwa na mamia ya watu wanaowafuatilia katika mtandao huo.

Kigwangala aliendeleza 'mashambulizi' kwa wizara hiyo: "Hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake?Hizi haziharibu mazingira? Cable inapita juu inaharibu mazingira gani? Zaidi ya ekari 350,000/- za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni risk kubwa? 'Watu wa mazingira' wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano tu?"

Baadhi ya watumiaji wa mtandao huo wa kijamii, kwa dhihaka wakamwandikia Makamba 'wapunguze makongamano.'

Hilo likamwibua Makamba ambaye alidai kuwa maelezo yake ndivyo ambavyo sheria inaelekeza na kusema hawezi kubishana hadharani na waziri mwenzake

"Baada ya kuona hilo jambo kwenye blogu, nikaeleza kile sheria inachotaka. Itakuwa ni jambo la kitoto kwangu, kumjibu, kujibizana ama kumshambulia waziri mwenzangu ambaye anataka kuboresha mambo kwenye sekta yake," aliandika Makamba.

Kigwangala baadae akaandika kuwa alilazimika kulijibia suala hilo mitandaoni kwa sababu liibuliwa mtandaoni, na kuwa toka hapo wasingeweza kukamilisha mradi huo bila kufanyika kwa tathmini ya mazingira.

Makamba mwishowe akawaasa watu kuacha kuendelea kuzungumzia na kupalilia jambo hilo mtandaoni kwani wote wanajenga nyumba moja: "...naomba hili jambo sasa liishe. Tunajenga nyumba moja, ya Watanzania. Hii ni kazi ya umma, na ya kupita. Leo upo, kesho haupo. Tulipoghafirika tumesameheana."

Leo Julai 8, 2019 Kigwangala pia amesema kuwa wamesameheana na kusisitiza kuwa Makamba hakutakiwa "kulileta" suala hilo kwenye mtandao wa Twitter.

Takriban watalii 50,000 hupanda mlima Kilimanjaro kila mwaka.

Wote hao wanakwea mlima huo mrefu zaidi barani Afrika kwa miguu, hivyo lazima awe ni mwenye afya njema.

Wizara ya Utalii nchini Tanzania inaamini kwa kuanzisha njia mpya ya kupandisha watu kileleni, idadi ya watalii wanaozuru kivutio hicho itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.

Updated: 09.07.2019 08:44
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.