Waziri Kalemani aipa Tanesco mwezi mmoja

Waziri Kalemani aipa Tanesco mwezi mmoja

17 June 2019 Monday 09:47
Waziri Kalemani aipa Tanesco mwezi mmoja


Na Teresia Mhagama, Dodoma 

WAZIRI wa Nishati, Dk Medadi Kalemani ametoa mwezi mmoja kwa  Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuwaunganishia umeme wateja wote waliolipia huduma hiyo na bado hawajaunganishiwa.

Pia ametoa hadi miezi sita kuanzia Julai, 2019 ushushaji umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ukamilike.

Ametoa maagizo hayo Dodoma katika mkutano wake na watendaji wa Tanesco na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mpango kazi kwa mwaka 2019/20 wa usambazaji umeme mijini na vijijini.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dk  Hamisi Mwinyimvua, Menejimenti ya TANESCO, REA na Bodi ya REA, pia ulijadili kazi zilizofanyika  mwaka 2018/19.

Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho ni upelekaji umeme viwandani,  kuimarisha hali ya umeme katika maeneo yaliyounganishwa na gridi, kuunganishia umeme taasisi za umma na maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme, bei ya kupeleka umeme vijijini, ununuzi vifaa vya umeme, utambuzi wa wateja wanaohitaji umeme viwandani na utambuzi wa wazalishaji wadogo wa umeme.

“ Kimsingi lazima tuhakikishe tunaimarisha huduma za umeme kwa kutatua kero mbalimbali kama za kukatika kwa umeme na kutowaunganishia umeme wateja ndani ya muda uliopangwa hivyo lazima tujipange sasa kukamilisha shughuli zetu kwa ukamilifu ili kuwezesha nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda,” alisema Dkt Kalemani

Suala la upelekaji umeme viwandani, Waziri wa Nishati, amesema kuwa ni la kipaumbele na ametoa miezi mitatu kwa Mameneja wa TANESCO wa Wilaya kuwasilisha takwimu ya viwanda walivyoviunganishia umeme kwenye maeneo yao.

Aidha, amewaagiza kuhakikisha wanafanya jitihada za kuunganishia umeme viwanda vinavyoanzishwa kwenye maeneo yao kabla havijakamilika kwa kupeleka bili stahiki kwa wenye viwanda ili waweze kufanya malipo mapema  na TANESCO kutoonekana kuwa ni chanzo cha kukwamisha ufanyaji kazi wa kiwanda.

kuhusu Wazalishaji wadogo wa umeme ameelekeza Mameneja wa TANESCO wilayani kuhakikisha kuwa, wanawatambua wazalishaji hao, wanawapa elimu, miongozo, wanawasimamia na kuwaingiza katika programu za uzalishaji umeme.

Kuhusu ununuzi wa vifaa vya umeme, Dkt Kalemani amesema mtendaji anapaswa kusimamia utekelezaji wa agizo la Serikali la kutonunua nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kurahisisha ufuatiliaji wa vifaa hivyo pia kuokoa muda mrefu ambao ungetumika kusafirisha vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.