Waziri Lugola:Dhamana itolewe ndani ya saa 24

Waziri Lugola:Dhamana itolewe ndani ya saa 24

02 October 2019 Wednesday 13:39
Waziri Lugola:Dhamana itolewe ndani ya saa 24

Na mwandishi wetu, Rukwa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesisitiza kuwa, dhamana zitolewe saa 24 nchini bila wananchi kuombwa rushwa na kwamba askari atakayepuuza agizo hilo, ataondolewa ndani ya Jeshi la Polisi.

Pia ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa, kuwasaka na kuwatia mbaroni wabakaji wanne waliokimbilia nchini Zambia.

Lugola amesema wabakaji hao lazima wakamatwe na waletwe nchini kwasababu Jeshi hilo lina mbinu zote za kuwasaka wahalifu hao wanaodaiwa kukimbia kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa baada ya kubainika kufanya uhalifu huo Wilayani Kalambo.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mji wa Matai wilayani Kalambo Mkoani humo, Lugola amesema Wilaya hiyo inakabiliwa na matukio mengi ya ubakaji ambapo mpaka sasa Polisi tayari imewatia mbaroni wabakaji 11 na bado hao wanne wanaendelee kutafutwa ili wakamatwe.

Lugola amesema kero alizopewa na wananchi hao katika mkutano wa hadhara zikiwemo ubakaji kuwa juu pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi kuachishwa masomo kwa ajili ya kufanyishwa kazi wakiwa na umri mdogo, pamoja na wanafunzi kubakwa na kupewa mimba.

“Haiwezekani wahalifu waichezee Serikali ya Rais Dkt. Magufuli, lazima wakamatwe, wasakwe kwa nguvu zote, na mnipe taarifa mtakapowatia mbaroni watuhumiwa hao,” amesema Lugola.

Aliongeza kuwa, wahalifu mbalimbali wakiwemo majambazi, kutokana na uimara wa Jeshi la Polisi wamesambaratishwa na wanaendelea kusakwa katika kona zote nchini mpaka jambazi wa mwisho atakapotiwa mbaroni.

Aidha, Lugola aliwataka wananchi kutoa taarifa kwake na kwa viongozi wa Polisi wa Wilaya na Mkoa endapo kuna mwananchi atabambikiziwa kesi au kuombwa rushwa wakati anamuombea dhamana ndugu yake.

Lugola alikiri kuwepo kwa baadhi ya polisi wanaoendelea kuwaomba rushwa wananchi ili wapate dhamana pamoja na kubambikiwa kesi.

“Ndugu wananchi, hili nilishaliagiza na pia naendelea kuliagiza, ni marufuku kwa askari polisi yeyote atakaye muomba rushwa mwananchi ili ndugu yake apewe dhamana, dhamana ni haki ya mwananchi, na uikiingia polisi bure na kutoka ni bure,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kalambo, Deokresi Mkandala alipokea maagizo ya Waziri Lugola likiwemo la kuwasaka wahalifu hao waliokimbilia nchini Zambia na kuahidi kuyafanyia kazi.

Waziri Lugola anaendelea na ziara yake Mkoani Rukwa kutatua kero mbalimbali za wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika Wilaya zote mkoani humo.

Updated: 02.10.2019 13:45
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.