Zitto aichambua hoja ya Magufuli kumfuta kazi January  

Zitto aichambua hoja ya Magufuli kumfuta kazi January  

22 July 2019 Monday 11:29
Zitto aichambua hoja ya Magufuli kumfuta kazi January  

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Kigoma mjini(ACT Wazalendo) Zitto Kabwe amesema ni bora Rais John Magufuli asingetoa ufafanuzi wa sababu za kumuondoa January Makamba katika nafasi ya uwaziri

Taarifa ya leo Julai 22, 2019 ya  kiongozi huyo wa ACT wazalendo inaeleza: Nimekusikia Rais leo ukijaribu kuelezea sababu za kumuondoa Uwaziri Bwana January Makamba. Kwa kweli hukuwa umejiandaa na maelezo ya kuridhisha.

Rais, kwenye suala la mifuko ya plastiki tunajua ukweli kwamba wewe ndiye ulizuia lisiendelee ulipoambiwa kwamba litaua viwanda. Tunajua kwamba January ndiye ametumia miaka mitatu kuwaandaa wenye viwanda vya mifuko ili wabadilishe teknolojia na wasipate hasara. Tunajua kwamba January alifanya vikao vya umma (public hearings) kuanzia Karimjee mwaka 2017 hadi Mwanza mwaka 2018 na kwingineko kushirikisha wananchi kwenye jambo hili. Tunajua kwamba hatukusikia kauli yako kwenye mifuko ya plastiki hadi baada ya suala hili kufanikiwa.  Hii sio kawaida yako maana wewe ni very predictable. 

Tunajua kwamba mlimtegea Makamba ili afeli halafu mumtimue. Hakufeli. Sasa mnamtimua kwa kukamilisha kazi kwa weledi mkubwa! Mhe Rais wewe ni mkali maelekezo yako yasipotekelezwa. Umemuachaje Waziri miaka minne kwa kutotii maelekezo halafu unamtoa baada ya utekelezaji? Hakuna mwenye akili timamu anayeweza kukubali hoja yako hii dhaifu sana. 

 Bwana Rais ulikutana na wafanyabiashara kote nchini kutwa nzima. Walitaja kero zao zote, nami nikaziorodhesha. Sikusikia hata mmoja akilalamikia NEMC. Kwasababu gani? Kwasababu January ameibadilisha NEMC. Alitaka kuibadilisha huko nyuma na akavunja bodi na kuondoa menejimenti lakini kwakuwa inasemekana kulikuwa na ndugu zako walioguswa ukaagiza uamuzi ule ubatilishwe. Unadhani Watanzania wamesahau? 

Bwana Rais fedha zinazotolewa na wahisani kwenye miradi ya mazingira zinakaguliwa na CAG na hakuna popote palipoonyesha ubadhirifu au upotevu. Kama upo uweke hadharani kama sisi tulivyoweka hadharani ubadhirifu wa TZS 1.5 Trilioni. Wacha wahisani, Serikali yako haijaweka hata senti tano kwenye miradi ya mazingira nchini. Mimi ni Mbunge na ninapitia kila Bajeti ya Serikali na Taarifa za CAG. Hujawahi kutenga fedha za Mazingira. Kwa kifupi, tunajua wewe binafsi sio mpenzi wa mazingira na umesema hivyo mara kadhaa. Hata huyo January mwenyewe “ulimtupa” kwenye mazingira ili apotee lakini ghafla kila Mtanzania leo anaongea mazingira. Hata wewe nawe leo unayaongea. 

Bwana Rais hulazimiki kutoa sababu unapomuondoa Waziri. Kwa kutafuta kutoa sababu zisizoshiba leo, umeonyesha kwamba umesikia hisia za Watanzania kuhusu kuondolewa January Makamba. Umeondoa Waziri kipenzi cha Watanzania na Waziri weledi. Tunajua umemfukuza kwasababu nyingine, sio uchapakazi. Watanzania wote tunajua kwamba siku zote alikuwa anatafutiwa sababu tu ya kuondolewa.  Ukisema uchapakazi ndio sababu Watanzania tunakushangaa kwasababu hawa mawaziri umewateua wewe lakini tathmini tunafanya sisi Watanzania. Na January Makamba ndiye alikuwa Waziri mbunifu na bora kabisa. Na ataendelea kuwa maarufu miongoni mwa Watanzania. Hakika ana nafasi kwenye uongozi siku sio nyingi sana zijazo. Mabadiliko ni lazima na January naamini atakuwa sehemu ya mabadiliko ili kujenga Tanzania inayojali watu wake na yenye Demokrasia iliyokomaa 

Updated: 22.07.2019 11:35
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.