Fainal Afcon 2019 ni Algeria vs Senegal

Fainal Afcon 2019 ni Algeria vs Senegal

15 July 2019 Monday 04:20
Fainal Afcon 2019 ni Algeria vs Senegal

Cairo, Misri
 Algeria na Senegal  zinakutana kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka 2019.

Timu hizo ambazo zilizanza mashindano katika kundi moja sawa na Tanzania na Kenya zimeibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao na kukata tiketi ya kukutana tena kwenye fainali.

Kwenye hatua ya makundi, Algeria iliilaza Senegal 1-0. Matokeo hayo yatajirudia Ijumaa usiku kwenye fainali hiyo

Goli la kujifunga la Tunisia katika muda wa nyongeza limewavusha Sengal mpaka hatua ya fainali ya kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) kwa mwaka 2019.

Nusu fainali ya kwanza ilizikutanisha Senegali na Tunisia.

Japo wengi waliipigia chapuo Senegal kushinda mchezo huo, lakini ushindi haukuwa rahisi.

Dakika 90 zilimalizika bila timu yoyote kupata ushindi, huku pande zote mbili zikikosa penati katika kipindi cha pili.
Ushindi ulipatikana kwa Senegal ndani ya dakika 30 za nyongeza.

Kipa wa Tunisia Moez Hassen alifanya makosa katika dakika ya 100 kwa kuokoa vibaya mpira wa krosi na kumgonga beki wake Dylan Bronn na kutinga wavuni.

Katika dakika za mwisho za mchezo huo kukatokea 'tafrani' baada ya refa kutoa penati golini mwa Senegal kwa madai kuwa kiungo Idrissa Gana Guaye ameunawa mpira.

Hata hivyo penati hiyo ilikataliwa baada ya refa kwenda kujihakikishia kwenye mwamuzi wa msaada wa televisheni (VAR).

Hii ni mara ya pili kwa Senegal kutinga hatua ya fainali. Mara ya kwanza ikiwa 2002 ambapo walipoteza kwa mikwaju ya penati dhidi ya Cameroon.

Safari ya Tunisia kutaka kulichukua kombe hilo kwa mara ya pili imetamatika mpaka hapo yatakapofanyika mashindano mengine.
Ilipotimu nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, nusu fainali ya pili baina ya Algeria na Nigeria ikaanza kutimua vumbi jijini Cairo.

Nigeria ndiyo timu pekee kati ya zilizocheza nusu fainali ambayo imeshinda kombe hilo zaidi ya mara moja. Imenyakua mara tatu, mara ya mwisho ikiwa 2013.

Hata hivyo usiku wa leo, ndoto zao za kuchukua kombe hilo kwa mara ya nne zimezimwa kwa kipigo cha goli 2-1 kutoka kwa mbweha wa jangwani, Algeria.

Algeria ilitangulia kuandika goli katika dakika ya 40 ya mchezo baada ya mchezaji wa Nigeria William Troost-Ekong kujifunga.

Nigeria wakarejea mchezoni kwa goli la kusawazisha lililofungwa kupitia mkwaju wa penati na Odion Ighalo katika dakika ya 73.

Mshambuliaji hatari wa Manchester City, Riyad Mahrez ndiye aliyepeleka kilio nchini Nigeria kwa kupachika bao la ushindi kwa Algeria katika dakika ya 95.

Algeria sasa ipo mbioni kulinyakua kombe hilo kwa mara ya pili.

Mara ya kwanza na ya mwisho kwao kulinyanyua kombe hilo ilikuwa 1990, hata Mahrez ambaye ni nahodha wa kikosi cha sasa alikuwa bado hajazaliwa.

Timu tatu zenye mafanikio makubwa zaidi Afrika - Misri, Cameroon na Ghana - ziling'olewa kwenye hatua ya mtoano au maarufu kama 16 bora.

Fainali itapigwa Ijumaa katika Dimba la Kimataifa la Cairo kuanzia saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.