Hawa hapa wapinzani wa Yanga, Simba, Azam, KMC barani Afrika

Hawa hapa wapinzani wa Yanga, Simba, Azam, KMC barani Afrika

22 July 2019 Monday 04:29
Hawa hapa wapinzani wa Yanga, Simba, Azam, KMC barani  Afrika

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Afrika, Simba SC, Yanga SC, Azam FC na KMC wote wataanzia hatua moja, Raundi ya Kwanza ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Afrika.  

Mabingwa wa Tanzania, Simba SC wataanza na UD do Songo ya Msumbiji katika Raundi ya kwanza ya mchujo wa kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika wakati watani wao, Yanga SC wataanza na Township Rollers ya Botswana.

Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Agosti 9 na 11 na Yanga SC itaanzia nyumbani Dar es Salaam, wakati Smba SC itaanzia ugenini na mechi za marudiano zitachezwa kati ya Agosti 23 na 25.

Pamoja na kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita Simba itaanzia Raundi ya kwanza. Julai 22, 2019 TFF kupitia mkurugenzi wa michezo atatoa ufafanuzi wa kwanini Simba inaanzia hatua hii.

Zikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na Yanga itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.

Ratiba hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika itailazimisha Simba SC kupanga tarehe nyingine ya tamasha lake la kila mwaka la kutambulisha kikosi kipya, Simba Day ambalo hufanyika Agosti 8, kwa sababu siku hiyo watakuwa Msumbiji kwa ajili ya mechi na UD do Songo.

Wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa, KMKM SC wao wataanzia nyumbani dhidi ya Desportivo de 1 Agosto ya Angola na wakivuka watakutana na mshindi kati ya Green Eagles FC ya Zambia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Katika Kombe la Shirikisho, Azam FC wataanzia ugenini na wawakilishi wa Ethiopia, wakati KMC itaanzia nyumbani Dar es Salaan dhidi ya AS Kigali ya Rwanda, timu mpya ya kiungo Haruna Niyonzima aliyewika na vigogo wa Tanzania Simba na Yanga kwa muongo wote huu.

Wakivuka mtihani huo, KMC watakutana na mshindi kati ya Proline FC ya Uganda anapotokea kocha wao, Jackson Mayanja na Masters Security Services ya Malawi wakati Azam FC itakutana na mshindi kati ya Triangle FC ya Zimbabwe na Rukinzo FC ya Burundi, anapotokea kocha wao, Ettiene Ndayiragijje.

Wawakilishi wa Zanzibar, Malindi SC wao wataanzia ugenini mjini Somalia dhidi ya Mogadishu City na wakiitoa watakutana na mwakilishi wa Misri.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.