banner68
banner58

Kegere, Morris kazi ipo

Kegere, Morris kazi ipo

12 July 2018 Thursday 17:55
Kegere, Morris kazi ipo

INAWEZEKANA gumzo la sasa kwa mashabiki wa soka ni mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2018 itakayopigwa Jumapili kule Moscow, Russia, lakini kabla hawajajua bingwa atakuwa nani, tayari wataishuhudia fainali nyingine kali ya Kagame 2018.

Ndio, kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam itapigwa fainali ya aina yake itakayoikutanisha mtetezi wa michuano hiyo, Azam dhidi ya Mabingwa wa kihistoria wa Kombe hilo, Simba waliopenya kwa mbinde jana mbele ya JKU.

Utamu sio timu hizo kukutana tu katika fainali ya 41 tangu michuano hiyo ilipoanza mwaka 1974, bali ni mkolezo wa nyota watakaokutana katika pambano hilo litakalotanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Singida United na Gor Mahia walionyolewa mabao 2-0 na Azam FC mapema jana mchana.

Simba imetinga hatua hiyo ikiwa fainali yake ya 12 na ya kwanza tangu walicheza mara ya mwisho mwaka 2011 walipocharazwa na Yanga bao 1-0 baada ya kuinyoa JKU kwa bao 1-0 katika pambano la nusu fainali lililopigwa jana Jumatano, jijini Dar.

Bao pekee la mchezo huo liliwekwa kimiani na Kagere kwa shuti kali akiwa ndani ya lango la JKU sekunde chache kabla ya mapumziko. Hilo lilikuwa bao la tatu la straika huyo aliyesajiliwa Msimbazi akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Katika mchezo huo, JKU iliwabana Simba kwa muda mrefu kabla ya kuruhusu bao hilo lililowang’oa katika nusu fainali, baada ya kudhani Kagere alikuwa ameotea.

Huku Kagere kule Morris

Baada ya Simba na Azam kupenya hadi fainali, mashabiki wa soka sasa wanasubiri kuona vita Kagere dhidi ya Nahodha wa Azam, Aggrey Morris ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa katika kikosi kilichobeba taji la Kagame mwaka 2015.

Morris amekuwa katika kiwango cha hali ya juu kwa muda mrefu na katika michuano hii ya Kagame amekuwa kikwazo kwa mastraika wasumbufu, jambo linalompa kazi Kagere kuanza kujipanga mapema kabla ya kukutana naye Jumapili.

Azam inayocheza fainali zake za tatu tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara mwaka 2008, ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia bila ya kuwepo kwa straika wake anayeongoza kwa mabao katika michuano hiyo, Shaaban Idd Chilunda.

Chilunda mwenye mabao saba alishindwa kucheza kwa kuhofiwa asije akaumia kabla ya kwenda kujiunga na Tenerife ya Hispania inayomsubiri ili aitumikie katika soka la kulipwa, lakini Ditram Nchimbi na Bruce Kangwa walimaliza kazi ndani ya dakika za nyongeza baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa suluhu.

Nchimbi alifunga bao la kuongoza dakika ya 92 kabla ya Kangwa kuongeza la pili dakika nane baadaye na kurejea ushindi uliowapa Azam taji la Kagame mwaka 2015 kwa kuicharaza Kogal’O idadi kama hiyo katika pambano la fainali lililopigwa Taifa.

Kutokana na ukuta wa Azam kulipwa na mtu wa kazi kama Morris akisaidiana na kina Abdallah Heri na Kangwa ni wazi mastraika wa Simba wakiongozwa na Kagere, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza wajipange kama wanataka kuipa timu yao taji la kwanza tangu walipotwaa mara ya mwisho mwaka 2002.

Simba nao wanapaswa kuanza kunoa makali ya kuhakikisha wanawazuia nyota wa Azam watakaokuwa wakiongozwa na Ramadhani Singano, Yahya Zayd, Paul Peter, Ditram Nchimbi na Joseph Mahundi ambao wamekuwa na uchu wa mabao.

Makocha wa pande zote mbili, Hans Pluijm wa Azam na Masoud Djuma sambamba na manahodha wa timu hizo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Morris wa Azam wametabiri litakuwa ni pambano kali Jumapili kutokana na rekodi zilizopo baina ya timu hizo.

Mwanaspoti

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.