banner68
banner58

Simba yachezewa sharubu na Ndanda FC Mtwara

Simba yachezewa sharubu na Ndanda FC Mtwara

15 September 2018 Saturday 20:48
Simba yachezewa sharubu na Ndanda FC Mtwara

MABINGWA watetezi, Simba SC leo wameshindwa kuendeleza ubabe wake kwa Ndanda FC baada ya kuambulia sare ya bila kufungana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Sare hiyo ya kwanza katika mechi ya kwanza ya ugenini baada ya kushinda mechi mbili mwanzoni nyumbani inamaanisha timu hiyo ya kocha Mbelgiji, Patrick J Aussems inafikisha pointi saba, wakati Ndanda FC inafikisha pointi nne katika mechi nne, baada ya kushinda moja awali na kufungwa mbili.

Aussems leo aliwaanzisha kwa pamoja washambuliai wake hatari, Nahodha John Bocco, Mnyarwanda Meddie Kagere mwenye asili ya Uganda na Mganda Emmanuel Okwi lakini wote wakashindwa kufurukuta mbele ya safu ya ulinzi ya Ndanda iliyoongozwa na Malika Ndeule.

Mchezo wa kujihami ulionekana kuisaidia Ndanda FC ambayo baada ya kufungwa na Simba SC katika mechi zote za nyumbani na ugenini tangu ipande Ligi Kuu mwaka 2014 leo imemaliza salama chini ya kocha wake, Malale Hamsini.

Pamoja na kusimama kama mshambuliaji pekee muda wote wa mchezo, lakini Vitalis Mayanga aliisumbua kidogo safu ya ulinzi ya Simba SC iliyoongozwa na Muivory Coast, Serge Wawa Pascal.  

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; bao pekee la mshambuliaji Abdalllah Ahmed ‘Shiboli’ dakika ya 90 na ushei kwa penalti limeipa ushindi wa 1-0 JKT Tanzania dhidi ya wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Na Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, bao pekee la Habib Hajji Kiyombo dakika ya 26 limeipa ushindi wa 1-0 Singida United dhidi ya KMC, wakati Mtibwa Sugar imepata sare ya 0-0 na Lipuli mjini Iringa kama ilivyotokea Uwanja wa Karume, Musoma mkoani ambako Biashara United imelazimishwa sare ya 0-0 na Kagera Sugar.

Tanzania Prisons imelazimishwa sare ya 2-2 na Ruvu Shooting Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Mabao ya Prisons  yamefungwa na Hassan Kapalata dakika ya 74 na Salum Kimenya dakika ya 89, wakati ya Ruvu yamefungwa na Khamis Mcha dakika ya 79 kwa penalti na Ayoub Kitala dakika ya 83.   

Mabingwa wa kihistoria, Yanga SC wao watateremka Uwanja wa Taifa kesho kuanzia Saa 10:00 jioni kumenyana na Stand United, huo ukiwa mchezo wao wa pili tu baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa; Diel Makonga, Aziz Sibo, Yassin Mustafa, Rajab Rashid, Abdallah Rajab, Malika Ndeule, Muhsin Mohammed/Ismail Mussa dk60, Baraka Gamba, Vitalis Mayanga, Hassan Nassor/Moshi Salum dk90+3 na Kiggi Makasi. 

Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mohammed Ibrahim ‘Mo’/Cletus Chama dk57, John Bocco, Meddie Kagere/Adam Salamba dk75 na Emmanuel Okwi/James Kotei dk59.  

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.