Waziri Mkuu Majaliwa ashudia Simba ikivutwa sharubu na Namungo FC

Waziri Mkuu Majaliwa ashudia Simba ikivutwa sharubu na Namungo FC

11 August 2018 Saturday 20:37
Waziri Mkuu Majaliwa ashudia Simba ikivutwa sharubu na Namungo FC

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba imelazimishwa suluhu na timu ya daraja la kwanza ya Namungo FC mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyeshudia mechi hiyo maalum kwa kuzindua Uwanja wa Majaliwa uliojengwa na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amezindua uwanja huo leo (Jumamosi, Agosti 11, 2018), na kuipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi huo.

Uwanja huo unajengwa katika kitongoji cha Mtichi kata ya Nachingwea na ndio utakaokuwa unatumiwa na timu ya Namungo FC kuchezea mechi za nyumbani.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema suala la ujenzi wa uwanja ni jambo muhimu na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linahamasisha ujenzi wa viwanja katika ngazi za mikoa na wilaya ili kutoa fursa kwa wananchi hususani vijana kushiriki katika michezo, hivyo amezitaka halmashauri nyingine ziige mfano wa wilaya ya Ruangwa.

 Akizungumzia kabla ya kuanza kwa mechi ya kirafiki kati ya timu za Simba na Namungo, Waziri Mkuu alisema “Michezo ni burudani na wananchi wanataka kuburudika, Simba chapeni kazi onyesheni uwezo wenu wa mwisho ili Namungo nao wapata ufundi.”.

 Pia alisema mbali na kucheza na Simba, timu hiyo ya Namungo inatarajiwa kucheza na timu ya Dodoma FC ya jijini Dodoma keshokutwa (Jumatatu, Agosti 13, 2018). Pia timu hiyo itacheza na Yanga na Azam za jijini Dar es Salaa hivi karibuni.

 Waziri Mkuu ametaja faida ya timu kama za Simba, Yanga, Azam na Dodoma FC kucheza na timu ya Namungo FC kuwa ni pamoja na kuwaimarisha wachezaji kwa kuwafanya wajiamini na kuondoa uoga wa kupambana na timu nyingine.

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza timu ya Namungo FC kwa hatua waliyofikia, kwani ilianza kwa kushiriki mashindano ya kugombea kuku, mbuzi na ng’ombe na sasa inashiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara. “Hakikisheni mnafikia lengo letu la kucheza Ligi Kuu,”.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kutokana na jitihahada za kuboresha maendeleo zinazofanywa na Mbunge wa jimbo la Ruangwa ambaye ni Waziri Mkuu, uongozi wa mkoa umeamua kuupa uwanja huo jina la Majaliwa ili kumuenzi.

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema hakuna uwanja Tanzania unaoweza kujaza watu 20,000 kwa mechi za kawaida nje ya Dar es Salaam na Mwanza. Nimeambiwa kulikuwa na tiketi 20,000 zimeisha zote.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.