Iran yaidungua ndege ya Marekani

Iran yaidungua ndege ya Marekani

20 June 2019 Thursday 12:34
Iran yaidungua ndege ya Marekani

Tehran, Iran

JESHI la Marekani limekiri Ndege yake kutunguliwa na jeshi la Iran ilipokuwa kwenye anga ya kimataifa kwenye eneo la mpaka kati ya ghuba ya Oman na Uajemi, maafisa wa Marekani wameeleza.

Pia Wanadiplomasia kutoka Marekani wametoa tahadhari kuhusu ndege za kibiashara ambazo zinaenda katika maeneo hayo kuwa ziko hatarini.
Awali vikosi vya kijeshi vya Iran vilidai kuwa vimeshambulia ndege ya kijasusi isiyo na rubani kwenye anga la Iran.

Vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti tukio hilo dhidi ya ndege isiyo na rubani walioiita RQ-4 Global Hawk, kusini mwa jimbo la Hormozgan.

Jeshi la Marekani awali halikuthibitisha kama ndege yake imeangushwa, huku msemaji akikana taarifa kuwa ndege ya Marekani ilikua kwenye anga la Iran.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya wizara ya ulinzi ya Marekani kusema kuwa watapeleka vikosi 1,000 zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kutokea mvutano kati ya Marekani na Iran.
Marekani iliishutumu Iran kushambulia kwa mabomu meli za mafuta katika Ghuba ya Oman.

Mzozo huo ulishika kasi siku ya Jumatatu wakati Iran iliposema kuwa itazidisha kiwango cha urutubishaji wa madini ya Urani kinyume cha makubaliano na mataifa yenye nguvu duniani mwaka 2015.

Iran imefikia uamuzi huo baada ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani.

Mgogoro ambao umekuwepo baina ya nchi hizo mbili tangu mwaka jana wakati rais Trump alipojitoa katika mkataba wa kimataifa wa mwaka 2015 uliolenga kumaliza mpango wa nyuklia nchini Iran.

Iran iliamua kuacha kutekeleza kile ambacho iliahidi kufanya mwanzoni mwa mwezi wa Mei na kutishia kuanza kutengeneza tena nyukilia.

Meli na ndege za jeshi zilizotumwa nchini Iran ambazo wafanyakazi wake sio wa dharura wametakiwa kuondoka.
 Siku ya Jumatatu, mkuu  wa Shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki (IAEA) Yukiya Amano alithibitisha kuwa Iran imeongeza uzalishaji wa madini ya kutengeneza silaha.

Lakini alikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo japo aliongeza kuwa hawajabainisha ikiwa madini iliyozalisha kufikia sasa imepita kiwango kilichowekwa.

Aliiambia Bodi ya usimamizi ya IAEA kuwa ni vyema Iran ihakikishe inatekeleza mkataba wa kimataifa wa nyukilia kikamilifu.

Wakati viongozi kutoka pande zote mbili wamesisitiza kuwa hawataki vita itokee, lakini bado mvutano ni mkubwa.

BBC

Updated: 20.06.2019 12:47
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.