Mvutano wazidi, Marekani na Iran

Mvutano wazidi, Marekani na Iran

25 June 2019 Tuesday 08:54
Mvutano wazidi, Marekani na Iran


Washington , Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa anaiwekea vikwazo vikali Iran ikiwemo ofisi ya kiongozi mkuu wa dini, Ali Khamenei.

Trump amesema vikwazo hivyo vya ziada ni kujibu hatua ya Iran kuiangusha ndege isio na rubani ya Marekani na mambo 'mengine mengi'.

Ayatollah Khamenei, ambaye ndio kiongozi mkuu nchini Iran amelengwa kwa kuwa ndiye anayehusika na hali ya uhasama katika utawala wa taifa hilo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohamed Javd Zarif amesema Marekani haipendelei diplomasia.
 
Pia  Zarif ameushutumu utawala wa Trump kwa kuwa na kiu ya vita

Hata hivyo waziri wa fedha nchini Marekani Steve Mnuchin alisema kuwa maagizo ya rais Trump ambayo yatazuia mabilioni ya madola ya mali ya Iran yalikuwa yanaandaliwa hata kabla ya Iran kuiangusha ndege ya Marekani isiokuwa na rubani katika Ghuba wiki iliopita.

Pia Wizara ya fedha nchini Marekani imesema kuwa makomanda wanane wa Iran ambao husimamia kitengo kinachoshauri vitendo vya jeshi kuu la {Islamic Revolution Guard Corps} IRGC wamo katika vikwazo hivyo vipya.

Pia zuio hilo litaunyima uongozi wa Iran kupata rasilimali za kifedha pamoja na kuwazuia  watu walioajiriwa na kiongozi huyo wa dini katika afisi kadhaa ama nyadhifa tofauti mbali na taasisi za kigeni za kifedha ambazo huwasaidia kufanya biashara.

Marekani imedai kwamba Ayatollah Khamenei ana utajiri mkubwa ambao unafadhili jeshi la IRGC.

Mwaka 2018 waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo alisema kwamba kiongozi huyo ana utajiri wenye thamani ya $95b ambao hutumika kulifadhili jeshi hilo.

Kwa nini Marekani inaweka vikwazo?
Mnamo mwezi Mei 2018, Ikulu ya Whitehouse ilirejesha vikwazo vyote ambavyo vilikuwa vimeondolewa dhidi ya Iran chini ya mkataba wa kinyuklia wa Iran ambao uliafikiwa na viongozi wa mataifa yenye uwezo mkubwa duniani ili kuizuia Iran kutengeza silaha zake za Kinyuklia.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili uliharibika mnamo mwezi Mei -mwaka mmoja baada ya Trump kujiondoa katika mkataba huo wa Kinyuklia , Marekani ilianzisha shinikizo dhidi ya Iran kwa kuziondolea ruzuku nchi ambazo zinanunua mafuta kutoka Iran.
Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulizi dhidi ya meli za mafuta katika Ghuba , ambayo Ikulu ya Whitehouse inasema kuwa Iran ndio ya kulaumiwa.

Tehran hatahivyo imekana madai hayo. Baadaye Maafisa wa Iran walisema kuwa taifa hilo litakiuka dhidi ya kiwango cha uzalishaji wa madini ya uranium yanayotumika kutengenezea silaha za kinyuklia.

Siku chache baadaye, ndege ya Marekani isiokuwa na rubani ilishambuliwa na majeshi ya Iran na kuangushwa katika kile ambacho Marekani inasema ni maji ya kimataifa , lakini Iran inasema kuwa ndege hiyo ilikuwa katika himaya yake.

Je vikwazo vya awali vimeiathiri vipi Iran?
Vikwazo hususan vile vilivyowekwa dhidi ya nishati , meli na sekta za kifedha -vilisababisha uwekezaji wa kigeni kupotea na kuathiri uuuzaji wa mafuta.

Vinazuia kampuni za Marekani kufanya biashara na Iran, mbali na kampuni za kigeni au mataifa yanayofanya biashara na Iran.
Hatua hiyo imesababisha uhaba wa bidhaa za kutoka nje ambazo hutengezwa na mali asili kutoka ugenini hususan nguo za watoto.

Kuanguka kwa thamani ya sarafu ya taifa hilo pia kunaathiri gharama ya chakula kutoka nchini humo kama vile nyama na mayai ambazo zimepanda bei.

Iran imejibu shinikizo hilo la Marekani kwa kusema kuwa inapanga kukiuka baadhi ya makubaliano ya mkataba wa kinyuklia.

Pia Iran imelaumu mataifa ya Ulaya kwa kushinda kuheshimu ahadi zake za kulinda uchumi wa taifa hilo dhidi ya vikwazo vya Marekani.

Je ndege isiokuwa na rubani ilifanywa nini?
Jeshi la Iran la IRGC lilisema kuwa kuangushwa kwa ndege hiyo isiokuwa na rubani ilikuwa ujumbe wazi kwa Marekani kwamba mipaka ya Iran ni hatari.

Lakini jeshi la Marekani linasisitiza kuwa ndege hiyo isiokuwa na rubani ilikuwa katika anga ya kimataifa katika mkondo wa bahari ya Hormuz wakati huo.

Amir Ali Hajizadeh , afisa mkuu katika jeshi la IRGC alisema kuwa ndege nyingine ya kijeshi iliokuwa ikibeba abiria 35 ilikuwa ikiruka karibu na ndege hiyo.

''Pia tungeiangusha hiyo pia, lakini hatukufanya hivyo'', alisema.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.