CCM yawataka wasanii kujitolea kutumbuiza shughuli za chama

CCM yawataka wasanii kujitolea kutumbuiza shughuli za chama

01 September 2018 Saturday 11:00
CCM yawataka wasanii kujitolea kutumbuiza shughuli za chama

Baada ya miaka mingi kuwatumia katika shughuli zake za chama huku ikiwalipa, CCM imeamua kuondokana na bajeti ya wasanii na wanamuziki.

Katika uongozi wa chama hicho uliopita, wasanii mbalimbali wakiwamo wa maigizo na Bongo Fleva walitumika katika majukwaa ya chama hicho kutumbuiza.

Hata hivyo, kauli aliyoitoa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally jana huenda ikakiweka mbali na wasanii wanaotaka kulipwa ndipo watumbuize, baada ya kueleza kuwa hawatakuwa na bajeti ya kuwanunua na kuwakodisha katika shughuli zao.

Akizungumza muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana mjini hapa, Dk Bashiru alisema milango iko wazi kwa wasanii wa fani zote ilimradi mchango wao uwe katika kujenga Taifa na si biashara.

“Hatutakuwa na bajeti kwa ajili ya kuwanunua na kuwakodisha wasanii, lakini milango iko wazi kwa wasanii wa fani zote ilimradi mchango wao katika shughuli zetu za kisiasa uwe ni kuwawezesha kufanya kazi na kujenga Taifa siyo biashara,” alisema.

Alitoa mfano wa John Komba alipoanzisha Kundi la ToT kuwa hakuwa akifanya biashara na kwamba alifariki dunia akiwa na maisha ya kawaida, lakini ameacha alama kubwa kwa Taifa na kimataifa.

ToT ni bendi inayomilikiwa na chama hicho. “(Komba) amekufa na maisha ya kawaida, hata familia yake inaishi maisha ya kawaida lakini ameacha alama kubwa. Wasanii kama Hadija Kopa hawafanyi kazi humu ndani (ya CCM) wakiwa wanalipwa fedha nyingi au kufanya biashara na kutajirika.”

Alisema, “sanaa kwa umuhimu wake wa kujenga Taifa haitakiwi kuwa bidhaa. Hatuna sababu ya kuwa na bajeti ya kuwakodisha wasanii. Lakini kuwawezesha kwa mafunzo, vifaa na usafiri ni lazima kwani watatembea kwa miguu mpaka maeneo yote?”

Hata hivyo, Dk Bashiru alisema kuwa hawatakuwa na mkataba wa kupanga bei ya kununua wasanii kama vile huduma nyingine kwenye shughuli za kisiasa.

“Lakini kuwa na mkataba na bei kwamba tukio hili tutapata milioni mbili, milioni tano, hapana. Wasanii kwenye chama kikubwa kama hiki ni wengi mno wapo wa ngoma za asili, mashairi, tamthilia, matambiko, mipira, maagizo,” alisema.

“Hakuna mradi wa kutumia sanaa kama chombo cha kukuza siasa yetu kwa kuwanunua wasanii au kuwakodisha kwa pesa kubwa.”

Alipoulizwa kuhusiana na bajeti ya kujikimu, Dk Bashiru alisema bajeti kwa ajili ya gharama za kujikimu kama usafiri, chakula na malazi hazina tatizo kwa sababu hata yeye amekuwa akilipwa mshahara na chama hicho.

“Hata mimi nalipwa mshahara hapa, lakini mshahara ambao utanifanya maisha yangu yawe ya staha. Siwezi kuja hapa kukilazimisha chama kinilipe mamilioni ambayo hakitaweza kuyamudu.”

“Hiyo ya kumkodisha (msanii) anatoka Mwanza anaenda Dodoma anakwenda wapi halafu anakuletea invoice (gharama) halafu unalipa milioni 10 milioni 20, hiyo hapana.”

Hata hivyo, alisema hana shida na maeneo ya wasanii wanaofanya kama zilivyo sekta za uzalishaji kwa kuuza sanaa zao kama bidhaa, lakini siyo katika siasa.

“Akina Ally Kiba hao. Nawapenda sana mie, lakini huko wanakoendelea na shughuli zao za kukuza vipaji vyao kama sekta ya uzalishaji nyingine za kuuza bidhaa ni sawa, lakini kama kuimba (ndani ya CCM) ni mchango wa Taifa,” alisema.

Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM, Dk Bashiru alisema msanii wa Afrika ni mwanamapinduzi, mpambanaji na mashairi ya nyimbo zake ni lazima yawe na hisia zinazowakera na kuwazomea wanyonyaji. “Yako wapi mashairi hayo, ziko wapi nyimbo hizo, ziko wapi ngoma hizo za kusifu bara letu na kuwakumbusha vijana bara hili liliwahi kutawaliwa?” alihoji.

“Ndio maana nimesema ndani ya CCM hatutakuwa na bajeti ya wasanii tena, tutabaki na TOT tutaimarisha chombo chetu kile kama alama na Vijana Jazz, basi. Tukienda Arusha tutawakuta wasanii kule wataimba mashairi, watacheza ngoma.”

Alisema alipopokewa makao makuu ya chama hicho aliburudishwa na vikundi vya ngoma lakini hamaanishi kuwa wasanii wa Bongo Fleva ni wabaya, isipokuwa ujumbe gani uliomo ndani ya sanaa hiyo.

Akizungumzia suala hilo, msanii Steve Nyerere alisema anajiandaa kukutana na Dk Bashiru kumweleza nguvu ya wasanii katika siasa akiamini kuna watu waliompotosha.

“Kwenye majukwaa ya wasanii leo kumekuwa na lawama nyingi wakishangaa pamoja na juhudi zao za kuwa makada watiifu wa CCM wanaambulia kuanza kubaguliwa. Imewanyong’onyesha sana kauli hiyo,” alisema Steve aliyewahi kuwa mratibu wa wasanii wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Pamoja na hilo la wasanii, Dk Bashiru pia alisema wanafuatilia majadiliano ya wanachama wao katika mitandao ya kijamii ili kujiridhisha kuwa haivuki mipaka ya uhuru walio nao. Alisema mitandao hiyo imekuwa chanzo cha fitina, kukebehiana na kuchafuana.

Alisema wakati mwingine mwenyekiti wa Taifa wa chama chao, Rais John Magufuli anachafuliwa katika mitandao hiyo na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa na UVCCM kulinda hadhi ya taasisi ya urais na chama.

Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.