Chadema washtushwa 'kukwama' zoezi la undikishaji wapiga kura

Chadema washtushwa 'kukwama' zoezi la undikishaji wapiga kura

19 September 2019 Thursday 06:48
Chadema washtushwa 'kukwama' zoezi la undikishaji wapiga kura

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

CHAMA cha Chadema kimeshtushwa na kukwama kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa baadhi ya maeneo nchini.

Hii hapa taarifa kamili ya chama hicho;

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu kinachoonekana ni kukwama kwa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Halmashauri ya Chato, mkoani Geita, bila kuwepo kwa taarifa yoyote rasmi kwanini shughuli hiyo haijafanyika kwa kadri ya maelekezo ya ratiba ya uandikishaji.

Kwa mujibu wa barua ya Juni 21, 2019 yenye Kumb. Na. EA/75/162/01A/158, iliyokuwa na kichwa cha habari, YAH; RATIBA YA UBORESHAJI YA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA, kutoka NEC kwenda kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, pamoja na mambo mengine, iliwasilisha ratiba kamili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ambapo ilionesha kuwa uandikishaji katika maeneo ya Mkoa wa Geita (Halmashauri ya Chato), Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Kigoma (kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mji wa Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Kakonko, Kasulu, Kibondo na) ulipangwa kufanyika Septemba 8, 2019 hadi Septemba 14, 2019. Shughuli hiyo haijafanyika hadi sasa, huku muda ukiwa umepita na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa vyama vya siasa, wadau wengine wa uchaguzi na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Vile vile, vikao vya awali na vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuapisha mawakala kwa Mkoa wa Kigoma (Halmashauri ya Uvinza), Mkoa wa Tabora, Katavi na Rukwa, bado havijafanyika kwenye halmashauri husika ili kujiandaa na shughuli ya uandikishaji iliyopangwa kuanza Septemba 21, 2019 hadi Septemba 29, 2019.

Kupitia taarifa hii, Chadema kinaitaka NEC kutoa ufafanuzi wa haraka, kwa umma, sababu za kukwama kwa uandikishaji katika maeneo yaliyotajwa hapo juu ili kuondoa mtanziko kuhusu hatma ya uboreshaji wa DKWK katika maeneo hayo na mengine yanayofuata. Aidha, Chadema kinaitaka NEC kutoa taarifa rasmi kwa wadau iwapo kuna mabadiliko yoyote (mengine) ya ratiba ili waweze kujiandaa ipasavyo kushiriki hatua hiyo muhimu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Chadema inaendelea kusisitiza wito wake kwa NEC kutambua unyeti wa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi mkuu, hivyo kwa kuwa ratiba ya awali ilitangazwa kwa umma, ni wajibu wa Tume kuutarifu umma kuhusu mabadiliko yoyote ya ratiba yanapotokea na sababu za mabadiliko hayo, kwa sababu Watanzania wana haki ya kujua ili pia waweze kujiandaa kushiriki zoezi hilo.

Imetolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene.

Updated: 19.09.2019 06:58
Comments
Avatar
Your Name
Post a Comment
Characters Left:
Your comment has been forwarded to the administrator for approval.×
<strong>Warning!</strong> Will constitute a criminal offense, illegal, threatening, offensive, insulting and swearing, derogatory, defamatory, vulgar, pornographic, indecent, personality rights, damaging or similar nature in the nature of all kinds of financial content, legal, criminal and administrative responsibility for the content of the sender member / members are belong.